Skip to content
Coat of arms of Tanzania

National Institute for Medical Research (NIMR)

Advancing Health Research, Enhancing Life

NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kupitia Mradi wa STEPPS (Strengthening Health System Capacity for Access and Delivery of Paediatric Praziquantel for Schistosomiasis in Tanzania) tarehe 18 Februari 2026 imezindua rasmi Utafiti wa utoaji wa dawa ya kichocho aina ya paediatric praziquantel kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, hatua inayopanua wigo wa matibabu kwa kundi ambalo kwa muda mrefu halikujumuishwa katika kampeni za utoaji dawa kwa pamoja. Uzinduzi huo umefanyika jijini Mwanza wakati wa Warsha ya Wadau ya kuanza kwa utoaji wa dawa hiyo chini ya Mradi wa STEPPS.
Akizindua rasmi utafti huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema hatua hiyo ni ya kihistoria kwa Tanzania, hasa baada ya nchi kuwa ya kwanza katika ukanda huu na huenda duniani kusajili dawa ya paediatric praziquantel. Ameongeza kuwa matokeo ya mwisho ya utekelezaji wa mradi huo yataisaidia Serikali kuiingiza dawa hiyo katika mwongozo rasmi wa utoaji wa huduma za afya nchini. Ameeleza kuwa ushahidi wa kisayansi uliokusanywa kwa zaidi ya muongo mmoja umeonesha kuwa watoto chini ya miaka mitano wanaoishi katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya kichocho wanaweza pia kuambukizwa, hali iliyosukuma juhudi za kutafuta mfumo maalumu wa dawa kwa kundi hilo la watoto chini ya miaka mitano. Aidha, amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada za kupambana na ugonjwa huo kupitia utoaji wa elimu kwa jamii, utekelezaji wa afua za kinga na tiba pamoja na kuboresha usimamizi wa maji katika maeneo yenye maambukizi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, amesema uzinduzi huo ni matokeo ya safari ndefu ya utafiti, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa ulioanza mwaka 2020 kupitia Mradi wa STEPPS. Amefafanua kuwa katika hatua ya utekelezaji, mifumo miwili jumuishi ya utoaji dawa—Test and Treat na Mass Drug Administration (MDA)—ilijaribiwa ili kubaini njia bora yenye ufanisi, gharama nafuu na inayokubalika zaidi kwa jamii kabla ya upanuzi wa kitaifa.
Naye Mtafiti Kiongozi wa mradi huo, Dkt. Paul Erasto Kazyoba, amesema tafiti zimeonesha kuwa watoto chini ya umri wa miaka mitano pia wana maambukizi ya kichocho, ilhali awali afua za dawa zililenga zaidi watoto wa umri wa kwenda shule kuanzia miaka sita. Ameongeza kuwa dawa hiyo imefanyiwa majaribio na imeonesha usalama na ufanisi kwa watoto wadogo, ikiwa na maboresho makubwa ikilinganishwa na dawa ya awali, ikiwemo kupunguza usumbufu uliokuwa ukijitokeza kwa baadhi ya watumiaji. Amesisitiza kuwa mradi huo umejengwa juu ya ushirikiano kati ya NIMR, Wizara ya Afya na washirika wa maendeleo wakiwemo UNDP, WHO/TDR na PATH, kwa ufadhili wa GHIT Fund ya Japan pamoja na END FUND.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa UNDP na Naibu Mwakilishi Mkazi wa Tanzania, Bw. John Rutere, amesema taasisi hiyo imeona umuhimu wa kushirikiana na NIMR, Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano wanapata dawa stahiki ya kutibu kichocho, akibainisha kuwa ushirikiano huo utaendelea si tu katika kudhibiti kichocho bali pia katika kushughulikia changamoto nyingine za afya ya jamii. Naye Bi. Grace Bahati, mkazi wa Kijiji cha Ishayahisho, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ameishukuru NIMR kwa mradi huo wa utafiti akisema utasaidia kubaini maambukizi ya kichocho mapema na kuwapatia watoto dawa, hatua itakayochangia kulinda afya ya jamii.
Warsha hiyo imewakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi kujadili mikakati ya kuongeza upatikanaji wa dawa hiyo nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki, sambamba na kuimarisha mifumo ya afya kwa ajili ya kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ifikapo mwaka 2030. Warsha hiyo ilitanguliwa na ziara ya kutembelea maeneo ambayo utafiti unafanyika, ikiwamo Hospitali ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ambapo wadau walijionea zoezi la utambuzi wa ugonjwa na ugawaji wa dawa likiendelea.

Section Title

CONGRATULATIONS

The National Institute for Medical Research (NIMR) extends its heartfelt congratulations to Dr. Nyanda Elias Ntinginya on his selection as a 2026 Kofi Annan Fellow in Global Health Leadership...

NIMR Launches DIMENSION Project to Advance Digital Innovation in Mental Health Care for People Living with HIV

NIMR Muhimbili Centre has launched DIMENSION (Digital Empowerment for Mental Health in Tanzania: Enhancing Healthcare Capacity through Innovative Digital Training Solutions for People Living with...

NIMR Receives Bioinformatics Equipment to Advance Health Research and Genomic Data Analysis

The National Institute for Medical Research (NIMR) has received bioinformatics equipment and systems from AMREF Health Africa Tanzania to advance health research and genomic data analysis, while...

NIMR YAONYESHA MATUMIZI YA UTAFITI KUBORESHA HUDUMA ZA VVU KWA MAMA NA MTOTO

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) umeonesha kwamba upimaji wa kiwango cha virusi vya VVU kwa mama wakati wa kujifungua unaweza kusaidia kuwatambua mapema...

SALAMU ZA POLE

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo...

Baraza la NIMR Lawataka Watafiti Kutumia Fursa Kuongeza Machapisho na Ubunifu

Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) limewataka watafiti kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika vituo vya Taasisi kuongeza machapisho na ubunifu wa utafiti, ili...

Serikali Yataka Tiba Asili Zenye Ushahidi wa Kisayansi Kujumuishwa Katika Mfumo Rasmi wa Afya

Serikali imetoa wito kwa watafiti na wadau wa tiba asili kuongeza kasi ya tafiti, uthibitishaji wa kisayansi na uwekezaji katika uzalishaji wa dawa za tiba asili, ili zenye ushahidi wa usalama, ubora...

Prof. Mdoe Asisitiza Kukamilishwa kwa Ukarabati wa Kituo cha NIMR Tukuyu

Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. James E. Mdoe, amesema ataendelea kushirikiana na Menejimenti ya NIMR katika kuhakikisha maeneo yaliyobaki ya...

NIMR na HJF Kuimarisha Ushirikiano wa Tafiti za Afya

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Henry M. Jackson Foundation (HJF) ya Marekani zimejadili namna ya kuendeleza ushirikiano katika tafiti za afya, ikiwa ni pamoja na kufanya...

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

Dira 2050