NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeendelea kuimarisha mfumo wa usimamizi wa fedha kwa kuendesha zoezi la kuandaa hesabu za miezi tisa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayolenga kuhakikisha uwajibikaji, usahihi wa taarifa za kifedha na matumizi bora ya fedha za umma.
Zoezi hilo linafanyika mjini Morogoro kuanzia tarehe 18 hadi 30 Mei 2026, likiwakutanisha wataalamu kutoka Idara ya Fedha na Uhasibu wa vituo vyote vya NIMR kwa ajili ya kupitia, kuhakiki na kuandaa taarifa za kifedha zitakazowezesha taasisi kuwa na mifumo madhubuti ya usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, amewapongeza wahasibu na wataalamu wa fedha kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha taasisi inaendelea kuwa mfano wa uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za umma.
Amesisitiza umuhimu wa kuandaa taarifa za fedha kwa umakini, weledi, usahihi na kwa wakati ili kuimarisha uwazi wa kifedha pamoja na kuhakikisha hoja za wakaguzi zinapatiwa ufumbuzi mapema na kwa ufanisi.
Prof. Aboud pia ametoa shukrani kwa wataalamu wa mifumo kutoka Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutoa usimamizi shirikishi pamoja na mchango wao katika kuboresha Mfumo wa Uhasibu wa Serikali wa MUSE, hatua inayochochea ufanisi, kasi na ubora wa upatikanaji wa taarifa za fedha Serikalini.
Wataalamu wa fedha na uhasibu wa NIMR wamesema maboresho ya Mfumo wa MUSE yatawezesha upatikanaji wa taarifa za fedha kwa haraka, kwa usahihi na kwa ufanisi zaidi, hatua itakayoimarisha usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma pamoja na kusaidia utekelezaji wenye tija wa shughuli za utafiti na huduma za afya nchini.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.