Waziri Mchengerwa Aipongeza NIMR kwa Tafiti Zinazoimarisha Huduma za Afya na Kuchochea Maendeleo ya Taifa
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameipongeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa mchango wake mkubwa katika kufanya tafiti na ubunifu unaoendelea kuboresha matibabu, kupunguza gharama za huduma za afya na kuimarisha mifumo ya afya nchini.Akifungua rasmi Kongamano la Kisayansi la 33 la NIMR lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Mhe. Mchengerwa aliyemwakilishi Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema Serikali inatambua mchango wa taasisi hiyo katika kusaidia kutambua, kutathmini na kuimarisha afua mbalimbali za kupambana na magonjwa huku matokeo ya tafiti yakiendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuboresha sera na huduma za afya kwa wananchi. Aidha, Mhe. Mchengerwa alisisitiza kuwa uwekezaji katika utafiti si anasa bali ni mkakati wa maendeleo ya taifa unaosaidia kujenga uwezo wa kutatua changamoto kwa ushahidi na ubunifu wa kisayansi, huku ukichochea maendeleo ya sekta mbalimbali na ukuaji wa uchumi.Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alisema kongamano hilo limefanyika wakati muafaka ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza sera ya Bima ya Afya kwa Wote, hatua inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha..Naye Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Prof. James Mdoe, alisema kwa zaidi ya miaka 40 taasisi hiyo imeendelea kufanya tafiti zenye mchango mkubwa katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, afya ya mama na mtoto, lishe, afya ya jamii na maeneo mengine ya kipaumbele.“Baraza la NIMR linaendelea kuunga mkono juhudi za Wizara ya Afya katika kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti yanatumika kikamilifu katika kuboresha sera, mipango na utoaji wa huduma za afya nchini,” alisema Prof. Mdoe.Akitoa taarifa ya taasisi, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, alisema kongamano la mwaka huu limekusanya watafiti, wataalamu wa afya, watunga sera na washirika wa maendeleo kujadili nafasi ya ushahidi wa kisayansi katika kuimarisha mifumo ya afya na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Prof. Aboud alisema NIMR imeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya kupitia tafiti zilizosaidia maboresho ya sera, huduma za matibabu, kinga dhidi ya magonjwa na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa tafiti za afya nchini. Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

