Kiwango cha ugonjwa wa usubi kwa watu wenye kifafa katika eneo la Mahenge, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro, kimepungua hadi asilimia 22, huku maambukizi kwa ujumla yakipungua kwa takribani asilimia 40, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa “Ubunifu wa Njia za Huduma za Kifafa Barani Afrika (EPInA)”.
Matokeo hayo yamewasilishwa katika mkutano wa siku mbili unaoendelea katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha wadau kutoka Wizara ya Afya, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Taasisi mbalimbali za Serikali, pamoja na washirika wa maendeleo kutoka Uingereza, Kenya na Ghana. Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kujadili matokeo ya utafiti uliofanyika Mahenge, mkoani Morogoro, na kuweka mikakati ya kuendeleza mapambano dhidi ya usubi na kifafa.
Akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekhalaghe, aliyemwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, amesema mafanikio hayo yanaonesha matokeo chanya ya ushirikiano kati ya Serikali, watafiti na jamii.
“Haya ni mafanikio makubwa ya jitihada za pamoja. Kupungua kwa kiwango cha maambukizi kwa asilimia 40 ni ishara kuwa tuko kwenye mwelekeo sahihi,” ameeleza Dkt. Shekhalaghe.
Aliongeza kuwa ili kutokomeza kabisa tatizo hilo, ni muhimu kuendelea na uimarishaji wa utoaji wa dawa hasa aina ya Ivermectin pamoja na kuongeza elimu kwa jamii.
“Niwaombe wananchi waendelee kushiriki kikamilifu katika matumizi ya dawa na kuamini wataalamu wa afya. Kifafa na usubi ni magonjwa yanayozuilika na kutibika,” alisisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dkt. George PrayGod, Meneja wa Kituo cha Utafiti cha NIMR Muhimbili amesema utafiti huo umetoa takwimu muhimu zitakazosaidia kuboresha sera na miongozo ya utoaji wa huduma za afya.
“Takwimu hizi ni msingi muhimu wa maboresho ya sera na mikakati ya afya ya umma, hususan katika maeneo yenye maambukizi ya usubi na kifafa,” alisema.
Kwa upande wake, Mtafiti Kiongozi wa EPInA, Dkt. Bruno Mmbando, alisema tafiti zinaonesha uhusiano wa karibu kati ya usubi na kifafa, ambapo maeneo yenye maambukizi makubwa ya usubi pia huwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kifafa.
“Mahenge bado ina changamoto kutokana na mazingira yake ya kijiografia yenye misitu inayochangia mazalia ya vimelea. Hata hivyo, tumeshuhudia mafanikio makubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma,” alisema Dkt. Mmbando.
Alibainisha kuwa maeneo ya Tukuyu (Mbeya) na Amani (Tanga) tayari yameonesha mafanikio makubwa zaidi, jambo linalotoa matumaini kuwa tatizo hilo linaweza kudhibitiwa kikamilifu.
Naye mshirika wa mradi wa EPInA kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, Profesa Charles Newton, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika mapambano hayo.
“Kama tulivyoweza kupiga hatua kubwa katika kudhibiti malaria, tunaweza pia kupunguza kwa kiwango kikubwa kifafa kinachohusishwa na usubi endapo tutaendelea kushirikiana kisayansi na kimkakati,” alisema Profesa Newton.
Utafiti wa EPInA ulitekelezwa Mahenge kwa lengo la kuimarisha huduma za kifafa kupitia maboresho ya kinga, uchunguzi wa mapema, matibabu na kuongeza uelewa wa jamii, ikiwa ni sehemu ya jitihada za muda mrefu za kupunguza na hatimaye kutokomeza usubi na kifafa nchini.
Section Title
NIMR Disseminates Impactful Research Findings at the 7th Africa Continental World AMR Awareness Week
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.








