Mwenyekiti mpya wa Baraza la Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. James Mdoe, amefurahishwa na kazi inayofanywa na Kituo cha Utafiti wa Dawa za Tiba Asili cha NIMR Mabibo katika kuendeleza tafiti za tiba mbadala kwa afya ya Watanzania.
Pongezi hizo alizitoa tarehe 24 Juni, 2025 alipofanya ziara ya kikazi kituoni hapo. Prof. Mdoe alitembelea kituo hicho kwa ajili ya kujitambulisha na kuona maendeleo ya tafiti, ugunduzi na uzalishaji wa tiba asili.
Akimkaribisha katika kituo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud alimpongeza Prof. James Mdoe kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi na kumuahidi kumpa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya Taasisi. Aliwasilisha taarifa ya kituo iliyoeleza mafanikio mbalimbali katika maeneo ya rasilimali watu, vitendea kazi, miundombinu ya majengo na maabara pamoja na maendeleo ya uzalishaji ya dawa za tiba asili. Akizungumza na watumishi wa kituo hicho, Mwenyekiti wa Baraza alielekeza Taasisi kuandaa mpango mkakati wa kutofautisha huduma na biashara, watafiti kuongeza machapisho ya tafiti, kusajili haki miliki, kuongeza ushirikiano na taasisi nyingine za tiba asili kama ITM na watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo ya Taasisi.
Prof. Mdoe alisisitiza kuwa tiba asili ni hazina muhimu inayoweza kutoa suluhisho la changamoto nyingi za kiafya na akahimiza juhudi zaidi katika kukuza ubunifu na utafiti katika eneo hilo. Pia alishukuru kwa mapokezi mazuri na kuahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi katika kuhakikisha kituo kinapiga hatua zaidi.