Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) leo, tarehe 8 Januari 2026, imeendesha mkutano wa majadiliano ya sera uliowakutanisha watafiti, watunga sera, watoa maamuzi wa sekta ya afya na wadau mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha matumizi ya ushahidi wa kisayansi katika kuandaa na kutekeleza sera zinazohusu maandalizi, kinga na mwitikio wa taifa dhidi ya magonjwa yanayolipuka na kurejea mara kwa mara.
Akifungua mkutano huo, Mgeni Rasmi Dkt. Ahmad Mohamed Makuwani, Mkurugenzi wa Huduma ya Afya ya Uzazi, Magonjwa ya Wanawake na Watoto kutoka Wizara ya Afya, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, amesema kuwa majadiliano hayo yanakuja katika kipindi muhimu kwa taifa, ambapo kumekuwa na kuendelea kushuhudiwa kwa milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, dengue, COVID-19 na Marburg. Amesema hali hiyo inaweka shinikizo kubwa kwa mifumo ya afya na hivyo kuhitaji sera zinazojengwa juu ya ushahidi madhubuti wa kisayansi.
“Mkutano huu ni jukwaa muhimu la kutafakari mazingira ya milipuko ya magonjwa nchini na kuimarisha uwezo wa pamoja wa taifa katika kuzuia, kugundua mapema na kukabiliana na vitisho vya afya ya jamii vya sasa na vya baadaye,” amebainisha Dkt. Makuwani. Ameongeza kuwa majadiliano ya sera ni nyenzo muhimu ya kuunganisha tafiti na maamuzi ya kisera ili kufanikisha uamuzi unaozingatia ushahidi.
Aidha, Dkt. Makuwani amesisitiza umuhimu wa kuimarisha tafiti za ndani, ikiwemo utafiti wa tiba asili, akibainisha kuwa uzoefu wa mlipuko wa UVIKO-19 umeonesha mchango wa tiba asili katika kupunguza madhara kwa jamii. Akitoa wito, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika tafiti za tiba asili na mifumo ya kitaifa ya utafiti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud, amesema kuwa mkutano huo umeandaliwa mahsusi kushughulikia masuala nyeti yanayohusiana na magonjwa yenye uwezekano wa kusababisha milipuko, huku ukilenga kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatafsiriwa na kutumika moja kwa moja katika sera na mipango ya kitaifa.
Prof. Aboud ameeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa la tafsiri ya maarifa, linalowaunganisha watafiti, watunga sera na watekelezaji ili kujadili ushahidi uliopo, kubadilishana uzoefu na kuandaa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha maandalizi, kinga na mwitikio wa taifa dhidi ya milipuko ya magonjwa.
“Tafiti zinaonesha kuwa maandalizi madhubuti dhidi ya milipuko yanategemea mifumo imara ya ufuatiliaji wa magonjwa, nguvu kazi ya afya iliyo imara na minyororo thabiti ya upatikanaji wa vifaa tiba,” ameongeza Prof. Aboud.
James Tumain Tengia, mwakilishi kutoka Wizara ya TAMISEMI, ameipongeza NIMR kwa kuandaa mkutano huo, akisema kuwa umefanikiwa kuwakutanisha watafiti, watunga sera na watoa maamuzi ili kuchakata matokeo ya tafiti mbalimbali na kuja na maoni yatakayosaidia kuboresha sera na miongozo ya utoaji wa huduma za afya.
Elizabeth Shayo, Mtafiti Mkuu kutoka NIMR, amesema kuwa mkutano huo umekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa umetoa fursa ya kujadili namna bora ya kupambana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kutokea nchini.
Akitoa majumuisho ya mkutano huo, Dkt. Ernest Mazigo, mtafiti kutoka NIMR na mratibu wa mdahalo huo amesema kuwa wadau ambao ni watunga sera na watoa maamuzi wamepokea mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na wameanza kuangalia namna ya kuyaingiza katika mifumo na utekelezaji wa sera za afya.
Mdahalo huo wa siku moja uliofanyika katika Ukumbi wa CEEMI, ofisi ndogo za NIMR jijini Dar es Salaam, ulijikita katika kuangalia namna ushahidi wa kisayansi unavyoweza kuboresha sera na miongozo ya utoaji wa huduma za afya nchini, pamoja na kubaini vipaumbele vya tafiti na mapungufu ya utekelezaji. Mdahalo huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa wataalamu kutoka Kurugenzi ya Kuratibu na Kukuza Utafiti ya NIMR akiwemo Mr. Emmanuel Makundi, Dkt. Stellah Kilima na Dkt. Elizabeth Shayo, huku Profesa Moshi Ntabaye aliyeendesha mjadala huo akishiriki kikamilifu katika kufanikisha mdahalo huo wa sera.
Section Title
NIMR Disseminates Impactful Research Findings at the 7th Africa Continental World AMR Awareness Week
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

















