Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeanza rasmi utekelezaji wa utafiti wa majaribio ya tiba ya kuharakisha kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha. Hayo yamebainishwa wakati wa kuendesha mafunzo ya siku mbili ya kutekeleza utafiti kwa watafiti na watoa huduma wa afya kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, yalifunguliwa rasmi na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Mwinjuma M. Mkungu. Katika hotuba yake, aliipongeza NIMR kwa kuwa kinara wa tafiti za afya nchini na kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya katika kuandaa tafiti zenye lengo la kumaliza kabisa magonjwa yanayosumbua jamii, hususani yale yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (NTDs).
โNIMR ni nguzo muhimu katika sekta ya afya kwa kuwa inatoa ushahidi wa kisayansi unaosaidia kupanga na kutekeleza afua bora. Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi hizo,โ alisema Mhe. Mkungu.
Mafunzo hayo yamefuatiwa na kuanza kwa uchukuaji wa sampuli kwa washiriki wa utafiti katika kijiji cha Ruaha, kata ya Mnazi Mmoja, Wilaya ya Lindi. Utafiti huu wa kisayansi unalenga kulinganisha tiba tofauti za magonjwa ya matende na mabusha, hususani dawa ya โDoxycyclineโ na โMoxidectin + Albendazoleโ, dhidi ya Kingatiba iliyopo sasa ya โIvermectin + Albendazoleโ.
Mtafiti Mkuu wa mradi wa utafiti kutoka NIMR, Dkt. Akili Kalinga, alisema kuwa tafiti hizi zinalenga kutafuta tiba mbadala na bora zaidi ambazo zitaweza kuharakisha kutokomeza ugonjwa huo nchini. โTumekuwa kwenye mapambano dhidi ya matende na mabusha kwa miaka mingi. Tunategemea kuwa utafiti huu utasaidia kuondoa kabisa vikwazo vinavyosababisha maambukizi ya Ugonjwa huu kuendelea katika baadhi ya maeneo.โ alisema Dkt. Kalinga.
Akizungumza wakati wa zoezi la uchukuaji wa sampuli, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruaha, Bi. Salima Kidamchong`we, alisema kuwa utafiti huo ni muhimu sana kwa jamii yao kwa sababu unawapa fursa ya kujua hali yao ya kiafya. โTunatoa shukrani kwa NIMR na Wizara ya Afya kwa kutuletea utafiti huu. Ni jambo la maana na lenye manufaa kwa wananchi wetu,โ alisema.
Naye mmoja wa washiriki wa utafiti kutoka kijiji cha Ruaha kata ya Mnazi Mmoja, Bw. Ali Bakari Natulama, aliipongeza NIMR kwa juhudi zake na kusema kwamba tafiti kama hizi zinasaidia sana katika kuelimisha jamii na kuwakinga na magonjwa hatari kama matende na mabusha.
Kwa sasa, ugonjwa wa matende na mabusha bado upo katika baadhi ya Halmashauri za wilaya nchini Tanzania ikiwemo Lindi Manispaa, Mtama, Mikindani, Kinondoni na Pangani. Licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa Halmashauri 114 kutokomeza maambukizi ya Ugonjwa na kusitisha ugawaji wa kingatiba uliofanyika kwa miaka mingi.
NIMR inatarajia kutumia matokeo ya utafiti huu kuboresha miongozo ya kitaifa na kidunia ya tiba na udhibiti wa magonjwa haya, kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya na wadau wengine.