Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. James Mdoe, leo tarehe 25 Julai 2025 amefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti cha NIMR Muhimbili, akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud.
Katika ziara hiyo, Prof. Mdoe ametembelea Maabara Kuu ya Kifua Kikuu, ambayo inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Kituo cha NIMR Muhimbili na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wa Wizara ya Afya. Maabara hiyo ni miongoni mwa nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini na kanda ya Afrika. Alisisitiza kuwa mwelekeo wa uongozi wake ni kuona NIMR inazidi kungโara kitaifa na kimataifa kupitia tafiti za afya zenye athari chanya kwa jamii.
Baada ya kutembelea maabara, Prof. Mdoe alipata nafasi ya kuzungumza na watumishi wa kituo hicho ambapo aliwatia moyo kuongeza tija na ubunifu katika kazi zao za utafiti, akisisitiza umuhimu wa kufikia malengo ambayo Taasisi imejiwekea. Aliahidi kushirikiana kwa karibu na menejimenti ya Taasisi katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Prof. Said Aboud alimpongeza Prof. Mdoe kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Baraza la NIMR.
Aidha aliwapongeza watumishi wa Kituo cha NIMR Muhimbili kwa mchango wao mkubwa katika kushiriki kutengeneza sera na miongozi ya tiba ya kifua kikuu na UKIMWI kitaifa na kimataifa kutokana na matokeo ya tafiti. Hata hivyo, aliwasihi kuongeza juhudi katika kuchapisha matokeo ya tafiti na kuandaa vijarida sera ili kuongeza ushahidi wa kisayansi kutoka katika kazi za utafiti wanazofanya. โKatika mwaka wa fedha 2024/25, tumefanikiwa kuchapisha machapisho 46 ya tafiti za afya katika majarida ya kitaifa, kikanda na kimataifa na vijarida sera 12 kutoka katika kituo cha NIMR Muhimbili. Hili ni jambo la kujivunia lakini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi,โ alisema Prof. Aboud.
Ziara hiyo imeonesha dhamira ya dhati ya uongozi wa juu wa NIMR katika kuimarisha usimamizi, kuongeza uwajibikaji na kuendeleza utafiti wa afya unaolenga kuboresha maisha ya Watanzania.