Wananchi wanaendelea kunufaika na huduma za tiba asili kupitia tafiti, na uanzishwaji wa kiwanda cha kuzalisha dawa za tiba asili cha NIMR Mabibo kufuatia juhudi kubwa za Serikali kuhakikisha dawa salama na zenye ubora zinapatikana kwa wingi nchini.
Akizungumza tarehe 29 Agosti, 2025 katika Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yaliyofanyika jijini Dodoma, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, aliipongeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa hatua kubwa zilizopigwa katika tafiti na uhamasishaji wa matumizi ya dawa za tiba asili.
Dkt. Kazungu alisema moja ya mafanikio makubwa ya NIMR ni uanzishwaji wa kiwanda cha Mabibo cha kuzalisha dawa za tiba asili ambacho kinatumia malighafi kutoka kwa wakulima wa miti dawa. โKiwanda hiki hakijaishia tu kuzalisha dawa salama na zenye ufanisi na ubora, bali pia kimetoa fursa za ajira kwa wananchi na kuongeza kipato kwa wakulima wa malighafi hizo,โ alisisitiza Dkt Kazungu.
Aidha, alitembelea banda la NIMR katika maonesho na kupongeza jitihada zilizofanywa huku akishauri kuimarisha tafiti zinazohusu tiba asili kwa magonjwa ya figo ambayo yanaongezeka kwa kasi katika siku za hivi karibuni.
Akitoa maelezo katika banda la NIMR Meneja wa kituo cha NIMR Mabibo Dkt. Emmanuel Peter alibainisha mchango wa NIMR katika kukuza tiba asili nchini kuwa ni pamoja na kufanya tafiti za tiba asili, kushiriki katika huduma jumuishi, kujenga kiwanda cha kuzalisha dawa za tiba asili, kuhamasisha tafiti, ugunduzi na matumizi ya dawa za tiba asili, kuimarisha ushirikiano na wadau wa tiba asili
Dkt. Peter alisema Kwa sasa, wananchi wanapata huduma jumuishi za tiba asili katika hospitali za rufaa za mikoa 14 ambapo mteja anaweza kuchagua tiba ya kisasa, tiba asili au kutumia zote kwa pamoja. โHuduma hii inamuwezesha mteja kufanyiwa vipimo vya kitaalamu na kupewa ushauri sahihi kuhusu tiba inayomfaa.
Maadhimisho hayo, yenye kaulimbiu โTuimarishe Huduma za Tiba Asili Zenye Ushahidi wa Kisayansi,โ yalianza tarehe 25 Agosti 2025 na yanatarajiwa kutamatika tarehe 31 Agosti 2025. Tukio hili limewakutanisha wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kutoka maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kubadilishana uzoefu, na kuhamasisha matumizi ya dawa za tiba asili kwa manufaa ya jamii.