Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa Kushirikiana na Wizara ya Afya, tarehe 18/08/2025 imeanza mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa maabara na watafiti kutoka taasisi mbalimbali za afya, lengo likiwa ni kuimarisha uwezo wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika kuchambua (Bioinformatics) takwimu za mpangilio wa vinasaba (NGS data) za magonjwa ya mlipuko zinazozalishwa nchini Tanzania, ili kutambua aina na kufuatilia mabadiliko ya vimelea hivyo vya maradhi.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tano yanayofanyika mjini Morogoro, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Vida Mmbaga, amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa maabara kutumia teknolojia ya kisasa katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
โKuchakata takwimu hizi kutasaidia kutoa usaidizi kwa nguzo zingine za udhibiti ambazo zinafanya kazi kwa pamoja na maabara, kwani kazi ya utabibu inategemea utambuzi kutoka maabara. Hivyo, wataalamu hawa wakiboresha uchambuzi wa kina, utaalamu wao utasaidia zaidi katika kudhibiti magonjwa,โ amesema Dkt. Mmbaga.
Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuboresha uchakataji wa takwimu za vimelea vya maradhi kwa usahihi ili kusaidia kudhibiti magonjwa kwa ufanisi na uhakika.
Naye Dkt. Clara Lubinza Mtafiti kutoka NIMR na Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Global Heath Security ambao NIMR inatekeleza kwa kushirikiana na Wizara ya Afya amesema mafunzo hayo yatawasaidia wataalamu wa afya na maabara kuweza kuvisoma vinasaba vya vimelea vya magonjwa, kuvielewa ni vimelea vya aina gani na kuvitambua vinapokua vinabadilika.
Aidha Dkt. Clara ameeleza kuwa matarajio baada ya mafunzo hayo ni kuhakikisha wataalamu wa afya wanapata uwezo wa kuchambua na kutambua vimelea vinavyosababisha magonjwa mbalimbali, kubaini tabia, aina na maeneo vinaposambaa, na kutambua mapema iwapo vitabadilika. โHatua hii itawawezesha watalaamu wetu kutoa taarifa kwa Wizara ya Afya kwa wakati, ili kuchukua hatua za haraka za kudhibiti na kuzuia usambazaji zaidi wa vimelea hivyo.โ Alieleza Dkt. Clara.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na NIMR kwa kushirikiana na Wizara ya Afya yamewakutanisha pamoja wataalamu kutoa NIMR, Wizara ya Afya, Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii, Hospital ya Magonjwa ya Mlipuko Kibong`oto, na Maabara ya Afya ya Jamii ya Zanzibar.