aasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeendesha mafunzo maalumu kwa watafiti vijana 13 kuhusu namna ya kuandaa maandiko ya tafiti za afya kwa madhumuni ya kuvutia washirika wa maendeleo kufadhili kazi za utafiti. Mafunzo hayo yalifanyika katika ofisi ndogo za NIMR, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 25 hadi 27 Juni 2025.
Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo watafiti chipukizi katika kuandaa mapendekezo ya tafiti yanayoweza kushindana kwa ajili ya kupata ufadhili wa kitaifa na kimataifa sanjari na kuwaandaa kuwa viongozi wa baadaye wa tafiti zenye tija kwa jamii.
Wakati huo huo, NIMR iliendesha Kambi ya Uandishi wa Makala za Kisayansi kwa watafiti 12, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taasisi wa kuongeza mchango wa watafiti wake katika jamii ya wanasayansi kupitia uchapishaji wa tafiti bunifu kwenye majarida ya kitaifa na kimataifa.
Hatua hizi ni mwendelezo wa juhudi za NIMR kuboresha uwezo wa rasilimali watu, kukuza ubora wa tafiti na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya sayansi na utafiti barani Afrika na duniani kote.


