Watumishi NIMR Wapatiwa Mafunzo ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Rushwa Mahali pa Kazi na Afya ya Akili
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeendelea kuonesha dhamira yake ya kujenga watumishi wenye weledi, uadilifu, uwajibikaji na afya njema kwa kuendesha mafunzo maalumu yanayolenga kuimarisha maadili ya utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa mahali pa kazi na kuhamasisha umuhimu wa afya ya akili.Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 18 Machi 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, yakiendeshwa na wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Prof. Said Aboud amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuimarisha utawala bora kupitia watumishi wa umma wanaozingatia maadili, sheria, kanuni na taratibu za kazi. Alisisitiza kuwa maadili ya utumishi wa umma ni msingi muhimu katika kujenga taasisi imara, yenye kuaminika na inayotoa huduma bora kwa wananchi.Prof. Aboud ameeleza kuwa NIMR inaongozwa na misingi mikuu mitano ya uendeshaji ambayo ni uadilifu, ujumuishwaji, ubora, uwajibikaji na uwazi, na kwamba mafunzo hayo yanalengs kuimarisha utekelezaji wa misingi hiyo katika kazi za kila siku za watumishi.Prof. Aboud amesema mafunzo hayo pia yataweka misingi ya maadili kwa watumishi wa umma na kujenga uzalendo kama njia mojawapo ya kuondoa vitendo vya rushwa mahali pa kazi.Sambamba na hilo, mtaalamu kutoka Taasisi ya Mirembe ametoa elimu kuhusu afya ya akili, akisisitiza kuwa ustawi wa akili ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija na ufanisi kazini. Alieleza kuwa mtumishi mwenye afya njema ya akili huwa na uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhimili changamoto za kikazi.Aidha, menejimenti ya NIMR imeisitiza kuwa itaendelea kujenga mazingira ya kazi yanayozingatia maadili, yasiyovumilia vitendo vya rushwa na yanayojali ustawi wa watumishi wote. Mafunzo hayo ya siku moja yaliyohudhuriwa na Menejimenti na watumishi wa NIMR kutoka makao makuu Dodoma na vituo vya utafiti yanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa NIMR na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii, sambamba na kuchangia juhudi za Serikali za kujenga utumishi wa umma wenye maadili na uwajibikaji. Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.
