ZAHRI na Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Wajifunza Mbinu za Mafanikio ya NIMR katika Utafiti wa Afya
Katika juhudi za kuimarisha utafiti wa afya visiwani Zanzibar, Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) kwa kushirikiana na Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, leo tarehe 15 Aprili, 2025, wamefanya ziara maalum ya mafunzo katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), ofisi ndogo ya Dar es Salaam, ikilenga kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za utafiti wa afya.Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Sabiha Filfil Thani, ambapo wajumbe walipata fursa ya kutembelea Maabara ya Utafiti wa Vinasaba vya Mbu Wanaoneza Malaria (Malaria Genomics Laboratory) na kujionea kazi mbalimbali za kisayansi zinazoendeshwa na watafiti wa NIMR.Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dkt. Mary Mayige ambaye ni Mkurugenzi wa Taarifa na Kurekebu Tafiti, alieleza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kufanya tafiti nyingi zenye tija kubwa kwa Taifa, ikiwemo zile zilizochangia moja kwa moja katika uundaji na uboreshaji wa sera za huduma za afya. Dkt. Mayige alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa taasisi za utafiti nchini ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazolikumba taifa.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Sabiha Thani, alisema kuwa ziara hiyo imewapatia maarifa na uelewa mpana kuhusu namna Taasisi ya NIMR inavyoendesha shughuli zake za utafiti kwa mafanikio. Alieleza kuwa Kamati yake itaishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza uwekezaji ZAHRI, hasa katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa, ili kuijengea uwezo wa kitaalamu katika kushughulikia masuala ya afya kwa ufanisi zaidi.Naye Khamis Rashid Kheir, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Tafiti na Usimamizi wa Maarifa kutoka ZAHRI, alisema kuwa ziara hiyo imelenga kujifunza kwa vitendo namna NIMR imeweza kujijengea msingi thabiti wa kitaaluma, kiteknolojia na kiutawala katika kufanikisha tafiti zake, pamoja na namna wanavyokabiliana na changamoto za utafiti katika mazingira ya kazi.Ziara hiyo imekuja ikiwa ni muendelezo wa juhudi za ZAHRI katika kujifunza na kuimarisha uwezo wake wa utafiti. Wiki chache zilizopita, Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar walifanya ziara ya kikazi katika Kiwanda cha Dawa za Tiba Asili cha NIMR kilichopo Mabibo, Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza kuhusu mchakato wa utafiti, uchunguzi na uzalishaji wa dawa mbalimbali za tiba asili kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya binadamu.