NIMR

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Said S. Aboud, ameridhishwa na maendeleo ya shughuli za utafiti na utoaji wa huduma za maabara yanayoendelea katika Kituo kidogo cha NIMR Gonja kufuatia ziara yake ya kikazi iliyofanyika tarehe 25 Februari 2026.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa uongozi wa Taasisi kutembelea vituo vyake nchini kwa lengo la kufuatilia utendaji kazi, maendeleo ya miundombinu pamoja na mchango wa tafiti katika kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Akiwa kituoni hapo, Prof. Aboud alikagua ukarabati wa majengo uliofanyika, maendeleo ya kitengo cha upimaji wa magonjwa mbalimbali kinachotumika katika tafiti pamoja na mifumo ya utunzaji na usimamizi wa takwimu zinazozalishwa katika maabara. Alielezwa kuwa maboresho hayo yamelenga kuongeza ubora wa huduma za uchunguzi wa magonjwa na kuimarisha mazingira ya kufanyia tafiti.
Akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu kuzungumza na watumishi, Mkuu wa Kituo cha NIMR Gonja, Ndugu Said Frank Magogo, alimshukuru Prof. Aboud kwa kuendelea kukipa kituo hicho ushauri wa kitaalamu, kuwapatia rasilimali watu, mashine za hematolojia na chemia hai pamoja na vitendanishi zilizochangia kuimarika kwa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya kituo katika kufanya tafiti na kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na wafanyakazi, Prof. Aboud aliwapongeza kwa kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuridhishwa kwake na maendeleo yaliyofikiwa hususan katika utoaji wa huduma za maabara kwa jamii pamoja na matumizi ya takwimu za tafiti katika kubaini maeneo mapya ya utafiti yanayolenga kutatua changamoto za afya nchini.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha matumizi sahihi ya takwimu zinazozalishwa kupitia tafiti ili kuongeza ushahidi wa kisayansi utakaosaidia kupanga na kuboresha afua za afya kwa Watanzania.
Ziara ya Mkurugenzi Mkuu katika Kituo cha NIMR Gonja ni sehemu ya juhudi za Taasisi za kuhakikisha vituo vyake vyote vinaendelea kuimarisha ubora wa tafiti, kuongeza ufanisi wa huduma za uchunguzi wa magonjwa na kutoa mchango endelevu katika maendeleo ya sekta ya afya nchini.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.