Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, ameielekeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuongeza idadi ya dawa za tiba asili zinazozalishwa na Kituo cha Utafiti cha NIMR Mabibo, ambazo utafiti wake umekamilika, ili zitumike katika huduma jumuishi zinazotolewa katika hospitali za rufaa za mkoa sita zaidi mbali na saba za sasa ili kuongeza huduma na kuisaidia jamii katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Mhe. Mhagama ameyasema hayo leo terehe 08/04/2025 alipotembelea banda la NIMR katika kilele cha maonesho ya Wiki ya Afya yaliyofanyika katika viwanja vya JKCC – Dodoma. Aidha, aliipongeza NIMR kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika utafiti wa afya, zinazolenga kutatua changamoto za kiafya kwa wananchi.
Aidha akieleza kuhusu mafanikio ya Tafiti, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Prof. Said Aboud alieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia tafiti za tiba asili zilizofanywa na taasisi hiyo. Alisema kuwa mpaka sasa, NIMR kupitia kituo chake cha Mabibo kimeweza kufanya tafiti za tiba asili ambazo zimeonyesha matokeo chanya na baadhi ya dawa zimeingizwa katika mpango wa huduma jumuishi.
Prof. Aboud amesema miongoni mwa dawa zilizofanyiwa utafiti ni pamoja PERSIVIN inayotibu tezi dume, WARBUGISTAT (Magonjwa nyemelezi), NIMREGENIN (Saratani), TANGESHA (Seli mundu), TMS 2001 (Malaria) na NIMRCAF (UVIKO-19) ambayo inaendelea kusaidia jamii kutibu magojwa ya mfumo wa upumuaji. Prof. Aboud amesema NIMR katika tafiti zake za hivi karibuni imefanikiwa kuja na njia mpya ya kugundua kifua Kikuu kwa njia ya kutumia sampuli za choo na damu pamoja na kupunguza dozi kwa wagonjwa wa kifua kikuu kutoka miezi 6 ya sasa hadi 4, kupunguza dozi ya chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kutoka dozi mbili hadi moja ambayo imerahisisha utoaji huduma na kupunguza gharama kwa Serikali.
“Kwa sasa mfumo wa kidijitali wa kuombea vibali vya tafiti za afya wa National Research Information Management System (NREIMS) umeimarishwa na unasomana na mfumo wa GePG katika kufanya malipo na TMDA katika tafiti za majaribio ya kitabibu yaani ‘Clinical Trials’. Pia mfumo huu unaweza kutoa vibali kwa njia ya kidijitali na hivyo kupunguza muda wa watafiti kupata vibali vya tafiti na ruhusa ya kuchapisha matokeo ya utafiti katika majarida ya kisayansi pale wanapoomba”. Amesema Prof. Aboud
Katika Wiki ya Afya, Taasisi pia ilitoa wasilisho la matokeo ya utafiti wa nchi nzima wa hali ya magonjwa yasiyoambukiza. Taarifa ambayo imetoa tathmini ya hali ya magonjwa yasioambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, figo, afya ya kinywa na meno na afya ya akili.
Akimshukuru Mhe. Waziri Prof. Aboud amesema kuwa NIMR iko tayari kufanya tafiti zaidi na kuongeza bidhaa za tiba asili katika huduma jumuishi ili kuendelea kuwasaidia watanzania kukabiliana na changamoto za kiafya
Maonesho hayo ya Wiki ya Afya yameandaliwa na Wizara ya Afya yakiwakutanisha pamoja wadau mbalimbali na Taasisi za Afya kwa ajili ya kujadili na kutathimini mafanikio na maendeleo ya afya nchini.