NIMR

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Simbachawene, ameipongeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa mchango wake mkubwa katika kufanya tafiti zinazogusa maisha ya Watanzania na kutoa bidhaa halisi zitokanazo na tafiti hizo, zenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali za kiafya.
Mheshimiwa Simbachawene ametoa pongezi hizo leo alipotembelea banda la NIMR katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma. NIMR inashiriki katika maadhimisho hayo kwa kuonesha kazi zake za utafiti, ikiwemo bidhaa za tiba asili pamoja na kutoa elimu kuhusu taratibu za kupata vibali vya kufanya tafiti za afya nchini.
Aidha Mhe. Simbachawene amesema kuwa ni jambo la kupongezwa kuona taasisi ya utafiti kama NIMR ikionesha bidhaa halisi zilizotokana na tafiti zake. Aliitaka NIMR kuhakikisha bidhaa hizo za tiba zinawafikia wananchi kwa kuzisambaza katika maduka makubwa ya dawa (pharmacy) katika kila mkoa.
“Imekuwa ni fursa nzuri kwa kuweka bidhaa hizi hadharani. Ninyi mnafanya tafiti na tafiti ndiyo zinawapa uhalali kuliko wengine. NIMR ni chombo cha taifa kwa ajili ya kuhakikisha ubora na usalama wa huduma hizi. Onenekaneni masokoni, zinapopatikana huduma hizi kama kwenye pharmacy kubwa kubwa kila mkoa. Ni jambo jepesi, mkifanya hivyo, sisi wananchi tutanunua tu,” amesema Mheshimiwa Simbachawene.
Kwa upande wake, Dkt. Akili Kalinga, Mtafiti Mkuu kutoka NIMR, amemshukuru Waziri kwa kutembelea banda la taasisi na kueleza kuwa NIMR imeendelea kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali ya afya yakiwemo magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, tiba asili, afya ya uzazi, lishe na mengineyo yenye lengo la kuboresha ustawi wa jamii.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma hufanyika kila mwaka kuanzia Juni 16, na kuhitimishwa Juni 23. Husherehekewa na Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi hao katika nchi zao. Maadhimisho huambatana na maonesho mbalimbali.