NIMR

Waganga na wataalamu wa tiba asili wametakiwa kuzingatia usalama na ufanisi wa dawa za tiba asili wanazozitoa kwa kuzipeleka katika vipimo vya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na NIMR ili kulinda na kuendelea kuboresha afya ya jamii na kuepuka madhara yanayotokana na matumizi holela ya dawa za tiba asili.
Hayo yamesemwa leo tarehe 31/08/2024 na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel katika Kongamano la Tatu la Kisayansi la Tiba Asili lilofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza ambapo limewakutanisha watafiti, wataalamu wa afya na waganga wa tiba asili zaidi ya 300 kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Dkt.Mollel amesema Serikali kupitia mamlaka zake inaandaa mfumo wa kuwatambua waganga na wataalamu wa tiba asili ili wajulikane, wafanye kazi zao kwa uwazi na kufuata maadili na sheria za nchi.
“Niwaombe wataalamu wetu ukishamuona mtu kwenye vyombo vya habari anaongea au anazungumzia dawa za tiba asili muiteni kwanza aeleze hicho anachokisema na akithibitishe na akishindwa muelekezeni aende kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na NIMR, hicho anachokifanya kiangaliwe ili apewe ushauri wa kisayansi akikataa kuna vyombo vya kuweza kushughulikia” amesema Mheshimiwa Dkt. Mollel
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Said Aboud ametoa wito kwa waganga wa tiba asili kufanya kazi kwa karibu na NIMR ili kuendeleza tafiti za tiba asili kwa lengo la kuwa na dawa zenye usalama, ufanisi na ubora.
Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili Prof. Hamisi Malebo ameiomba Serikali Kuiongezea NIMR bajeti ya utafiti wa tiba asili kwa kuwa ina uwezo wa kufanya utafiti wa usalama na ufanisi wa dawa zaidi ya 100 kwa mwaka kama itawezeshwa na bajeti ya Serikali.
Kongamano hilo la kisayansi la tiba asili huandaliwa na NIMR kwa kushirkiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali hufanyika kila mwaka tarehe 31 Agosti likiwakutanisha watafiti, wataalamu na waganga wa tiba asili kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi kuwasilisha na kujadili matokeo mbalimbali ya tiba asili.