Skip to content
Coat of arms of Tanzania

National Institute for Medical Research (NIMR)

Advancing Health Research, Enhancing Life

NIMR

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) umeonesha kutorejea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Usubi (Onchocerciasis) katika eneo la maambukizi la Tukuyu kwa kipindi cha miaka minne ya ufuatiliaji tangu utafiti wa awamu ya kwanza ulipobaini kupungua maambukizi na kupendekeza kusitishwa kwa utoaji wa dawa za kingatiba kwa jamii mwaka 2021.Kuthibitishwa kuendelea kusitishwa kwa maambukizi inaotoa matumaini mapya katika juhudi za kutokomeza ugonjwa huo katika eneo hilo na baadaye nchi nzima.
Matokeo hayo yaliwasilishwa Oktoba 15, 2026, katika warsha iliyowakutanisha watoa huduma za afya, Maafisa wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, watafiti na wadau wengine kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe kujadili ushahidi wa utafiti na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kudumisha mafanikio yaliyofikiwa.
Akitoa matokeo hayo, Mtafiti Mkuu kutoka NIMR, Dkt. Akili Kalinga, amesema vipimo vya haraka vya kingamwili aina ya Ov16 vilionesha kiwango cha maambukizi kisichozidi asilimia 0.1 kama shirika la afya Duniani WHO linavyopendekeza miongoni mwa watoto wa miaka kuanzia mitano hadi tisa katika kipindi chote cha miaka minne (2022-2025) ya ufuatiliaji. Aidha, uchunguzi wa Inzi weusi wanaosambaza ugonjwa huo haukubaini Inzi yeyote kuwa na maambukizi katika sampuli takribani 6,000 zilizochunguzwa kila mwaka.
Amesema utafiti huo ulilenga kutathmini hali ya maambukizi baada ya utekelezaji wa afua za udhibiti na kubaini kama eneo la Tukuyu lenye halmshauri za wilaya nne (Busokelo, Ileje, Kyela na Rungwe) lilikuwa limefikia vigezo vya kusitisha utoaji wa dawa za kinga kwa jamii na baadaye kuthibitisha kutokomezwa kwa maambukizi
Dkt. Kalinga ameongeza kuwa matokeo hayo yanatoa msingi wa kupanga hatua zinazofuata za ufuatiliaji wa kutokomeza maambukizi kwa miaka mitatu ijayo 2027-2030.
Aidha, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP), Dkt. Clarer Jones Mwansasu, amesema hatua inayofuata ni kuandaa nyaraka za ushahidi wa kutokomeza ugonjwa (elimination dossier) zitakazowasilishwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya uhakiki, sambamba na kuandaa mkakati wa kuzuia kurejea kwa maambukizi.
Vilevile amesema kuna umuhimu wa kuwa na afua jumuishi za kudhibiti magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele katika mfumo wa kawaida wa utoaji huduma za afya, badala ya kuzitegemea programu maalumu pekee. Amezitaka Halmashauri na mikoa kutenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza afua hizo na kuimarisha uendelevu wa juhudi za kudhibiti haya magonjwa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo, Dkt. Joseph Ligoha, amesema matokeo hayo yamepokelewa kwa furaha na matumaini makubwa kwa kuwa yanaonesha maendeleo katika juhudi za kutokomeza ugonjwa wa Usubi, ambayo ni sehemu ya malengo ya Serikali katika kuboresha afya ya wananchi.
Dkt. Ligoha ameishukuru Serikali na NIMR kwa kuwezesha utafiti na kuwasilisha matokeo yake, akieleza kuwa ushahidi huo unaongeza hamasa kwa viongozi na watumishi wa afya kuendeleza juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.
Matokeo haya yanasisitiza umuhimu wa kuendeleza utafiti wa kisayansi, ufuatiliaji wa maambukizi na mipango ya afya katika ngazi za mikoa na halmashauri ili kulinda mafanikio yaliyofikiwa na kuimarisha juhudi za kutokomeza Usubi.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

Dira 2050