Serikali imetoa wito kwa watafiti na wadau wa tiba asili kuongeza kasi ya tafiti, uthibitishaji wa kisayansi na uwekezaji katika uzalishaji wa dawa za tiba asili, ili zenye ushahidi wa usalama, ubora na ufanisi ziweze kujumuishwa katika mfumo rasmi wa afya nchini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, katika Kongamano la Tano la Kisayansi la Tiba Asili lililofanyika leo, tarehe 28 Agosti 2026, katika Ukumbi wa Eden Highlands Hotel, Jijini Mbeya, ambapo alimwakilisha Naibu Katibu Mkuu – Dawa na Vifaa Tiba wa Wizara ya Afya, Mhe. Emanuel Tayari, aliyekuwa Mgeni Rasmi.
Balozi Dkt. Ulisubisya amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa maliasili na maarifa ya tiba asili ambayo yanaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto mbalimbali za afya, iwapo yatafanyiwa tafiti za kutosha na kuthibitishwa kisayansi.
Amesema Serikali inahitaji kuona ongezeko la tafiti za tiba asili, uwekezaji katika maendeleo ya dawa hizo pamoja na kuimarika kwa uzalishaji katika viwanda vya ndani.
Aidha, ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya wanasayansi, wataalamu wa tiba asili, wataalamu wa afya, taasisi za udhibiti, vyuo vikuu, watunga sera na sekta nyingine, ili kujenga mfumo unaowezesha tiba asili zenye ushahidi kutumika kwa usalama ndani ya huduma rasmi za afya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Prof. James E. Mdoe, amesema maendeleo ya tiba asili yanahitaji kujenga daraja kati ya sayansi ya kisasa na maarifa ya jadi yaliyorithishwa na jamii kwa vizazi.
Prof. Mdoe amesema Kongamano hilo ni fursa kwa watafiti, wataalamu wa tiba asili, watunga sera, watoa huduma za afya na wadau wengine kujadili ushahidi uliopo, changamoto na fursa za kuendeleza tiba asili nchini.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, amesema Taasisi hiyo kupitia Kituo cha Utafiti wa Tiba Asili Mabibo imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya maabara kwa ajili ya kuimarisha msingi wa kisayansi wa dawa za tiba asili.
Prof. Aboud amesema maabara hizo tayari zinatumika kufuatilia ubora wa dawa 45 zinazopatikana kupitia mpango wa huduma jumuishi, ambapo dawa hizo zimewafikia zaidi ya wagonjwa 2,000 katika hospitali 14 za rufaa za mikoa.
Prof. Aboud pia amesema NIMR inakamilisha taratibu za kuhakikisha Kiwanda cha Dawa za Tiba Asili Mabibo kinafunguliwa rasmi katika mwaka wa fedha 2026/27.
Kongamano hilo, lenye kaulimbiu “Kuongeza Kasi ya Ujumuishaji wa Tiba Asili Zenye Ushahidi wa Kisayansi Katika Mifumo Rasmi ya Afya: Jukumu la Ushirikiano wa Sekta Mbalimbali,” limewakutanisha wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala, watafiti, watoa huduma za afya, watunga sera, taasisi za udhibiti, vyuo vikuu na washirika wa maendeleo.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.













