Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. James E. Mdoe, amesema ataendelea kushirikiana na Menejimenti ya NIMR katika kuhakikisha maeneo yaliyobaki ya ukarabati wa Kituo Kidogo cha Utafiti cha NIMR Tukuyu yanakamilishwa.
Prof. Mdoe ametoa kauli hiyo Agosti 27, 2026, wakati wa ziara ya siku moja katika Kituo cha Utafiti cha NIMR Mbeya na Kituo Kidogo cha Utafiti cha NIMR Tukuyu, ikiwa ni sehemu ya kujionea shughuli za utafiti zinazoendelea katika vituo hivyo pamoja na hali ya miundombinu na mazingira ya kazi.
Akiwa Tukuyu, Prof. Mdoe alielezwa na uongozi wa Kituo cha Utafiti cha NIMR Mbeya kuwa ukarabati wa kituo kidogo hicho unaendelea kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato vya Taasisi. Prof. Mdoe alisisitiza umuhimu wa kukamilisha maeneo yaliyosalia ya ukarabati.
Ziara hiyo pia ilimpa Prof. Mdoe fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za utafiti zinazofanyika katika vituo hivyo, ikiwemo tafiti za Kifua Kikuu na Virusi vya UKIMWI katika Kituo cha NIMR Mbeya, pamoja na tafiti za ugonjwa wa Usubi zinazofanyika katika Kituo Kidogo cha Utafiti cha NIMR Tukuyu.
Katika Kituo cha Utafiti cha NIMR Mbeya, Prof. Mdoe alitembelea maabara za utafiti na kujionea matumizi ya mitambo ya kisasa kwa ajili ya shughuli za utafiti, pamoja na miundombinu ya kuhifadhi sampuli na majengo yanayotumika katika shughuli za kituo.
Akizungumza na watumishi wa NIMR Mbeya na Tukuyu, Prof. Mdoe aliwatia moyo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na weledi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya kazi ili kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Prof. Mdoe pia amewataka wananchi kushiriki katika tafiti zinazofanywa na NIMR, akieleza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuwezesha tafiti kuzalisha ushahidi wa kisayansi unaoweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za afya zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Utafiti cha NIMR Mbeya, Dkt. Bariki Mtafya, amemshukuru Prof. Mdoe kwa kutembelea vituo hivyo na kupata fursa ya kujionea shughuli za utafiti pamoja na changamoto zinazowakabili watafiti.
Dkt. Mtafya amesema uongozi wa kituo utaendelea kushirikiana na Menejimenti ya NIMR katika kushughulikia changamoto mbalimbali na kuhakikisha shughuli za utafiti zinaendelea kwa ufanisi.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.











