Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imefanya mkutano tarehe 21 Mei 2025 kwa ajili ya kuwasilisha matokeo ya utafiti wa tathmini ya maambukizi ya ugonjwa wa Usubi katika eneo la Tukuyu. Eneo hilo linajumuisha halmashauri za wilaya ya Kyela, Busokelo, Rungwe, Ileje na Ludewa.
Mkutano huo wa siku moja umefanyika katika Wilaya ya Kyela na kuwahusisha viongozi wa Serikali za Mitaa, wataalamu wa afya, wawakilishi wa Wizara ya Afya na watafiti kutoka NIMR.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Mhe. Katule Kingamkono ambaye alikuwa mgeni rasmi ameipongeza NIMR na Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa walizofanya katika kupambana na ugonjwa wa Usubi kwa zaidi ya miaka 20.
Amesema kuwa hatua ya kusitisha umezeshaji wa dawa kwa wananchi ni ishara ya mafanikio makubwa baada ya kushuka kwa kiwango cha maambukizi. “Tunaishukuru NIMR kwa kuendelea na tathmini ya kina ili kupata majibu ya uhakika yatakayowezesha kutangaza rasmi kutokomezwa kwa ugonjwa wa Usubi katika eneo hili” amesema Mhe. Kingamkono.
Aidha, ametoa wito kwa madiwani, maafisa tarafa, watendaji wa kata na vijiji, wenyeviti wa vijiji, wahudumu wa afya na wadau wengine kushirikiana kikamilifu na wataalamu wa afya wakati wa utekelezaji wa tathmini ya mwisho ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Mtafiti Mkuu kutoka NIMR, Dkt. Akili Kalinga, amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kuwafahamisha wananchi kuhusu maendeleo ya utafiti wa tathmini ya maambukizi ya Usubi baada ya kusitishwa kwa umezeshaji wa dawa za kingatiba uliodumu kwa miaka 21.
“Tathmini ya awali ilionesha kuwa maambukizi yameshuka hadi kufikia kiwango cha chini karibu na asilimia 0.01 – kiwango kinachopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya kutangaza kutokomezwa kwa ugonjwa,” amesema Dkt. Kalinga. Aliongeza kuwa tathmini ya mwisho itakayofanyika sasa itaelekeza kama ni lazima kuendelea na ugawaji wa dawa au kutangaza rasmi kuwa ugonjwa huo umetokomezwa katika eneo la Tukuyu.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Bi. Toyi V. Midaba kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa Wizara imeandaa mikakati maalum ya kufuatilia magonjwa kama Usubi ambayo awali hayakuwa yanapewa uzito ili kuhakikisha yanatokomezwa kabisa.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ushirika, Andendekisye Jeremia Mwakalinga, ameishukuru NIMR kwa kutoa elimu na kushirikisha jamii katika matokeo ya utafiti huo. Amesema taarifa hizo zitasaidia kuwapa matumaini wananchi walioteseka na ugonjwa huo kwa miaka mingi.
Mkutano huo umehudhuriwa na madiwani wa Halmashauri za Kyela na Ileje, waganga wakuu wa wilaya, maafisa wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, watafiti wa NIMR, wataalamu wa afya, maafisa elimu, maafisa tarafa, watendaji wa kata, wenyeviti wa vijiji na watendaji wa vijiji kutoka wilaya ya Kyela na Ileje.