NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imetoa matokeo ya awali ya Utafiti kuhusu vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza (NCD) nchini Tanzania. Utafiti huo ulifanyika kuanzia mwezi Septemba hadi Novemba 2023 kupitia mradi wa STEPS NCD Survey uliofadhiliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya.
Matokeo hayo yamewasilishwa na Mtafiti Mkuu wa mradi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taarifa na Kurekebu Tafiti, NIMR Dkt. Mary Mayige katika mdahalo wa kitaaluma uliohusisha wadau mbalimbali wa afya, kwenye maadhimisho ya Wiki ya Afya. Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya JKCC – Dodoma kuanzia tarehe 3 hadi 8 Aprili 2025.
Dkt. Mayige amesema kuwa Utafiti huo wa kina ulikuwa na lengo la kutathmini hali ya afya ya watu wazima wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 18 hadi 69 kwa kutumia hatua tatu kuu: ukusanyaji wa taarifa za kijamii na tabia za kiafya, vipimo vya mwili (urefu, uzito na shinikizo la damu), na vipimo vya kimaabara kupima sukari, figo na kolesteroli katika damu.
Aidha Dkt. Mayige amesema matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa bado kuna tatizo la magonjwa yasiyoambukiza nchini Tanzania ikiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu, afya ya akili, afya ya kinywa na meno na magonjwa mengine yasiyoambikiza.
Dkt. Mayige amesema kuwa takwimu zinatoa taswira ya kina ya hali ya vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza miongoni mwa watu wazima wa Tanzania amabapo amesisitiza haja ya dharura ya kuimarisha afua za afya ya umma ili kukabiliana na vihatarishi hivyo na kuboresha afya ya Watanzania kwa ujumla.
NIMR ni miongoni mwa Taasisi za afya zilizoshiriki Wiki ya Afya Kitaifa. Mbali na kuwasilisha matokeo ya utafiti pia imeshiriki maonesho ya Wiki ya Afya kwa kutoa elimu ya kupata vibali vya utafiti, kuonesha bidhaa za tiba asili zilizofanyiwa utafiti katika kituo cha utafiti wa tiba asili Mabibo.