Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa maadili ya tafiti za afya nchini kwa kuweka mfumo thabiti wa kitaifa wa ithibati kwa Bodi za Maadili za Utafiti za Taasisi (Institutional Review Boards – IRBs).
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Prof. Said Aboud wakati wa ufunguzi wa mkutano wa ngazi ya juu wa mashauriano na Bodi za Maadili za Utafiti uliofanyika Oktoba 26, 2026, katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya NIMR jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umejadili namna ya kuimarisha udhibiti wa tafiti za afya na utekelezaji wa mfumo wa kitaifa wa ithibati na uimarishaji wa Bodi hizo.
Prof. Aboud ameeleza kuwa kuongezeka kwa tafiti za afya, zikiwemo majaribio ya kitabibu, tafiti za vinasaba na tafiti zinazohusisha taasisi nyingi, kunahitaji mfumo madhubuti wa udhibiti unaolinda haki, utu, usalama na ustawi wa washiriki wa tafiti.
Amesisitiza kuwa kulinda imani ya wananchi kunahitaji kuhakikisha kila utafiti unaofanyika nchini, ukusanyaji wa sampuli za kibaolojia na matumizi ya takwimu za afya vinaongozwa na viwango vya juu vya maadili, uwazi na uwajibikaji.
Akitoa muhtasari wa mfumo wa uratibu na udhibiti wa tafiti za afya nchini, Mkurugenzi wa Taarifa na Kurekebu Tafiti NIMR na Katibu wa NatHREC Dkt. Mary Mayige, amesema kuwa mapitio ya maadili ya tafiti nchini hufanyika katika ngazi ya kitaifa kupitia Kamati ya Kuratibu Utafiti wa Afya (MRCC) na Kamati ya Taifa ya Maadili ya Utafiti wa Afya (NatHREC) na katika ngazi ya taasisi kupitia Bodi za Maadili za Utafiti za Kanda au Taasisi (Z/IRBs/IRECs).
Dkt. Mayige ameeleza kuwa NatHREC ina jukumu la kupitia ubora wa kisayansi na kimaadili wa mapendekezo ya tafiti, kulinda haki na usalama wa washiriki, pamoja na kusimamia masuala yanayohusu uhamishaji na ushirikishwaji wa takwimu na sampuli za utafiti.
Akiwasilisha mada kuhusu mchakato wa ithibati ya Bodi za Maadili za Utafiti nchini, Mkuu wa Kitengo cha Kurekebu Tafiti za Afya na Naibu Katibu wa NatHREC, Dkt. Obadia Bishoge, ameeleza kuwa tathmini ya ithibati inahusisha uhakiki wa nyaraka zilizowasilishwa na taasisi pamoja na ukaguzi wa mazingira na miundombinu ya Bodi husika.
Amesema kuwa tathmini hiyo huzingatia upatikanaji wa ofisi na miundombinu inayofaa, vifaa vya kusaidia usimamizi wa mapitio ya kimaadili, watumishi wenye sifa katika sekretarieti, muundo wa uongozi wa Bodi, mipango ya mafunzo na kujenga uwezo, huduma za usaidizi kutoka taasisi husika pamoja na ubora wa taratibu za kawaida za uendeshaji (SOPs).
Mkutano huo wa siku moja ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya mifumo ya kitaifa ya udhibiti wa tafiti za afya na Bodi za Maadili za Utafiti katika ngazi za taasisi, kwa lengo la kuhakikisha tafiti zinafanyika kwa kuzingatia maadili na viwango vinavyotakiwa
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.





