Katika kuimarisha ushirikiano na jamii, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) tarehe 29/05/2025 imekutana na timu ya viongozi kutoka kata mbili zinazozunguka kituo cha utafiti cha NIMR Gonja.
Ujumbe huo ulioongozwa na Mheshimiwa Issa Jasper Rashid, Diwani wa Kata ya Maore, ulihusisha Mtendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji na Wenyeviti wa Vitongoji 11. Viongozi hao walitembelea kituo cha NIMR Gonja na kujionea maendeleo makubwa ya ufufuaji wa kituo hicho.
Wameipongeza NIMR kwa hatua hiyo muhimu na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika shughuli za utafiti sanjari na kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii juu ya shughuli zitakazotekelezwa kituoni hapo.
Mkuu wa kituo cha NIMR Gonja, Bw. Said Frank Magogo, aliwashukuru viongozi hao kwa kutambua umuhimu wa kutembelea kituo hicho, akibainisha kuwa wao kama wawakilishi wa wananchi ni wadau muhimu wa Taasisi. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya NIMR na jamii unachagiza mafanikio ya Taasisi katika kutekeleza jukumu lake kuu la kufanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kuboresha afya ya Watanzania.
Akijibu maombi ya viongozi hao waliotaka tafiti zaidi zifanyike juu ya magonjwa kama homa ya ini ambayo imeisumbua jamii hiyo kwa muda mrefu, Bw. Magogo alieleza kuwa ushirikiano wa karibu na jamii huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuibua maeneo mapya ya kufanya tafiti za afya. Aliahidi kuwa NIMR itaendelea kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha utafiti unagusa mahitaji halisi ya jamii.