Skip to content
Coat of arms of Tanzania

National Institute for Medical Research (NIMR)

Advancing Health Research, Enhancing Life

NIMR

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) umeonesha kwamba upimaji wa kiwango cha virusi vya VVU kwa mama wakati wa kujifungua unaweza kusaidia kuwatambua mapema mama na watoto walio katika hatari kubwa ya maambukizi, huku ubunifu wa kidijitali ukichangia kuboresha upatikanaji wa majibu ya vipimo katika vituo vya huduma za afya.
Ushahidi huo umetokana na miradi ya LIFE na LIFE2Scale inayofadhiliwa na EDCTP, iliyolenga kuboresha huduma kwa wajawazito wanaoishi na VVU na watoto walio katika hatari ya kuambukizwa. Matokeo hayo yaliwasilishwa tarehe 10 Septemba 2026 katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi 2026, uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kwa ajili ya kuwafikishia watunga sera na wadau wa afya ushahidi wa kuendeleza maboresho ya miongozo na huduma za afya.

Akifungua mjadala huo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said S. Aboud, amesema tafiti hizo zimeonesha umuhimu wa upimaji wa kiwango cha virusi vya VVU kwa mama wakati wa kujifungua katika kuwatambua walio katika hatari kubwa ya maambukizi na kuhakikisha wanaohitaji huduma wanafikiwa mapema.
Prof. Aboud amesema NIMR imefanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, TAMISEMI na wadau, huku ikitumia na kuimarisha mifumo ya kitaifa iliyopo badala ya kuanzisha mifumo sambamba.

Naye Mtafiti Mkuu wa LIFE2Scale, Dkt. Issa Sabi, amesema utafiti wa LIFE uliofanyika Tanzania na Msumbiji kati ya mwaka 2019 na 2022 ulionesha kuwa upimaji wa kiwango cha virusi vya VVU kwa mama wakati wa kujifungua unaweza kutambua mama na watoto wengi zaidi walio katika hatari kubwa ya maambukizi kuliko kutegemea vigezo vya kitabibu pekee. Amesema LIFE2Scale ilijengwa juu ya ushahidi huo kwa kuingiza ubunifu huo katika huduma za kawaida na kuimarisha mifumo ya kitaifa ikiwemo Electronic Sample Referral System (ESRS) na Unified

Dkt. Sabi amesema utekelezaji wa LIFE2Scale katika vituo vya afya vya Mbeya na Songwe umechangia kuboresha mifumo ya utoaji huduma, ikiwemo kuongeza uwezo wa upimaji kupitia ununuzi wa takribani mashine 15 za GeneXpert kwa ajili ya upimaji wa VVU kwa watoto wachanga na magonjwa mengine, ikiwemo kifua kikuu. Amesema NIMR imewasilisha matokeo hayo kwa watunga sera na wadau wa afya ili kuchochea matumizi mapana ya ushahidi huo na kuendeleza maboresho yaliyopatikana katika maeneo yaliyoshiriki utafiti.

Killian Mlalama alieleza namna Unified Community System–Kituoni App (UCS-Kituoni), iliyounganishwa na ESRS, ilivyosaidia kupunguza utegemezi wa majibu ya vipimo kwa njia ya karatasi na kuchangia kuboresha muda wa upatikanaji wa majibu, hususan katika vituo vya huduma vinavyopokea huduma kutoka vituo vya upimaji.

Kwa upande wa Wizara ya Afya, Dkt. Mukome Nyamhagatta, Mratibu wa Taarifa za Kimkakati katika Mpango wa Taifa wa Kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (PMTCT), amesema Serikali imeona manufaa makubwa ya utafiti huo katika kutoa ushahidi unaoweza kusaidia kuboresha miongozo ya utoaji wa huduma za afya, na kuishukuru NIMR kwa kuendelea kutekeleza miradi yenye ushahidi unaosaidia Tanzania kuboresha utoaji wa huduma.
Amesema Tanzania imepiga hatua katika kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na upimaji wa VVU kwa watoto wachanga, lakini bado kuna umuhimu wa kuimarisha ufuatiliaji wa kiwango cha virusi vya VVU kwa wajawazito, upimaji wakati wa kujifungua, upimaji wa VVU katika vituo vya huduma na matumizi ya taarifa katika kuboresha huduma.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

Dira 2050