NIMR

Wataalamu kutoka idara mbalimbali za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), wakiongozwa na Idara ya Manunuzi na Ugavi wamekutana kuandaa Mpango wa Manunuzi wa mwaka wa fedha 2025/26 kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija katika Taasisi.

 

Akizungumza leo tarehe 29 Mei 2025 alipotembelea timu ya washiriki wa kuandaa mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud amesisitiza umuhimu wa kuwa na Mpango wa Manunuzi wa Mwaka ulioandaliwa kwa ushirikishwaji wa idara tumizi na umakini mkubwa ili kuweza kuutekeleza kwa wakati na kufikia malengo ya Taasisi. Amewakumbusha washiriki kuandaa mpango wenye uhalisia, kuzingatia sheria ya manunuzi ya umma na kanuni zake na kuchakata maombi kupitia mfumo wa NeST. “Mpango wa manunuzi wa mwaka ukiandaliwa na kutekelezwa vizuri unawezesha Taasisi kufikia malengo yake ya mwaka kwa wakati,” amesema, Prof. Aboud huku akiwapongeza watumishi kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika, uadilifu na weledi.

 

Mkutano huo wa kuandaa Mpango wa Manunuzi wa Mwaka unaofanyika mjini Morogro ulianza tarehe 26 na unatarajia kumalizika 30/05/2025 ambapo umewakutanisha maafisa manunuzi, bajeti, TEHAMA, watafiti wanasayansi, Meneja wa Manunuzi na Ugavi, Meneja wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Makao Makuu, Kituo cha Muhimbili, Tanga, Amani, Korogwe, Mbeya na Mwanza na Mbeya.