NIMR

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud, tarehe 21 Juni 2025, amefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti cha NIMR Tabora, kwa lengo la kukagua maendeleo ya miradi ya miundombinu na kuhimiza uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa ajili ya kuongeza ufanisi na tija katika tafiti.
Katika ziara hiyo ya siku moja, Prof. Aboud amepokea taarifa ya maendeleo kutoka kwa Mkuu wa Kituo hicho, Dkt. Calvin Sindato, kuhusu miradi inayoendelea ikiwemo ukarabati wa jengo la utawala na ujenzi wa uzio wa kuzunguka kituo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na kuboresha mazingira ya kazi. Baada ya maelezo hayo, Prof. Aboud alitembelea eneo la ujenzi na kujionea hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza na watumishi wa kituo hicho, Prof. Aboud alisema kuwa uboreshaji wa miundombinu ni sehemu ya mkakati wa kitaasisi wa kukifanya Kituo cha Tabora kuwa miongoni mwa vituo vya mfano nchini katika utoaji wa suluhisho la changamoto za kiafya kwa kutumia ushahidi wa kisayansi.
“NIMR itaendelea kuwekeza katika miundombinu, vifaa vya kisasa vya utafiti, mafunzo ya kuwajengea uwezo na motisha kwa watumishi”. “Lengo letu ni kuhakikisha tafiti zetu zinaleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi na kushawishi sera za afya” amesema Prof. Aboud.
Kituo cha NIMR Tabora kilianzishwa mwaka 1922, na ni miongoni mwa vituo kongwe zaidi vya utafiti wa afya nchini. Kituo kimekuwa na mchango mkubwa katika tafiti za kudhibiti ugonjwa wa Malale (Human African Trypanosomiasis) hususan katika maeneo yenye hatari kubwa ya maambukizi nchini Tanzania.
Katika miaka ya hivi karibuni, kituo hiki kimepanua wigo wa tafiti zake kwa kutumia mtazamo wa Afya Moja (One Health) unaojumuisha afya ya binadamu, wanyama, na mazingira. Vipaumbele vya tafiti za sasa katika kituo hiki ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya, homa za virusi za kutokwa damu, magonjwa yanayosambazwa na mbu pamoja na vimelea vya maradhi na ufuatiliaji wa vinasaba kwa vimelea vinavyoweza kusababisha milipuko ya magonjwa.
Kituo kimeanza kutumia teknolojia rahisi na inayobebeka ya upimaji wa vinasaba kwa ajili ya kugundua mapema na kukabiliana na milipuko ya magonjwa. Teknolojia hii inasaidia kuongeza uwezo wa taifa katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya milipuko na hivyo kulinda afya ya jamii.
Ziara ya Prof. Aboud imetoa msukumo mpya kwa maendeleo ya kituo cha NIMR Tabora. Kupitia uwekezaji katika miundombinu, vitendea kazi, rasilimali watu na teknolojia, NIMR inaendelea kujidhihirisha kama taasisi ya kimkakati katika kukabiliana na changamoto za afya kwa kuzalisha ushahidi wa kisayansi kuanzia ngazi ya jamii hadi kimataifa.