Skip to content
Coat of arms of Tanzania

National Institute for Medical Research (NIMR)

Advancing Health Research, Enhancing Life

NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Henry M. Jackson Foundation (HJF) ya Marekani zimejadili namna ya kuendeleza ushirikiano katika tafiti za afya, ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za pamoja, kuimarisha uwezo wa watafiti na kutumia miundombinu iliyopo kupanua wigo wa tafiti nchini.
Majadiliano hayo yalifanyika tarehe 13 Agosti 2026 katika Kituo cha Utafiti cha NIMR Mbeya, wakati Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa HJF, Meja Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Marekani, Dkt. Joseph Caravalho, pamoja na ujumbe wake walipotembelea kituo hicho.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, alisema kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Serikali ya Tanzania na Marekani kunatoa fursa ya kuendeleza ushirikiano katika tafiti za afya, hasa wakati ambapo mazingira ya ufadhili wa tafiti za afya duniani yanaendelea kubadilika.
Prof. Aboud alisema NIMR imewekeza katika miundombinu ya utafiti katika Kituo cha Mbeya na vituo vyake vingine, ikiwemo maabara na vifaa vinavyowezesha tafiti mbalimbali za afya.
Katika majadiliano hayo, pande hizo pia zilizungumzia mabadiliko katika ufadhili wa utafiti kutoka Marekani. Prof. Aboud alitoa shukrani kwa Serikali ya Marekani kwa mchango wake kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR), ambao umeunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya VVU na changamoto nyingine za afya ya umma.
NIMR na HJF pia zilijadili maeneo ya ushirikiano wa baadaye, yakiwemo kuendeleza tafiti za pamoja, kujenga uwezo wa watafiti na kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano wa kisayansi.
Baada ya majadiliano, ujumbe wa HJF ulitembelea Maabara ya Usalama na Kinga ya Mwili (Safety and Immunology) ya Kituo cha NIMR Mbeya, ambapo ulijionea shughuli za utafiti zinazotekelezwa katika kituo hicho. Ujumbe huo pia ulielezwa kuhusu uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo HJF, katika kuimarisha miundombinu ya kituo.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa pande zote mbili kueleza utayari wa kuendeleza ushirikiano uliopo na kutumia miundombinu na uwezo wa watafiti kupanua tafiti za afya nchini.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

Dira 2050