Skip to content
Coat of arms of Tanzania

National Institute for Medical Research (NIMR)

Advancing Health Research, Enhancing Life

NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Kituo cha Mbeya, imetumia Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) Kanda ya Kusini kuwafikia wananchi moja kwa moja, hususan wakulima ambao ni sehemu kubwa ya washiriki katika tafiti zake, kwa kutoa elimu ya afya, huduma za uchunguzi na elimu kuhusu tafiti za afya zinazofanyika katika Kanda ya Kusini.
Maonesho hayo, yaliyofikia kilele tarehe 8 Agosti 2026, yalitoa fursa kwa Taasisi kuimarisha uhusiano na jamii na wadau mbalimbali, huku likiwafikia kundi muhimu la wananchi wanaoshiriki katika tafiti zake. Takriban asilimia 90 ya washiriki katika tafiti zinazofanywa katika kituo hicho ni wakulima, hivyo Nanenane imekuwa jukwaa muhimu la kuwafikia moja kwa moja na kuwaeleza umuhimu wa ushiriki katika tafiti zinazolenga kuboresha afya na ustawi wa jamii.
Kupitia banda la NIMR, wananchi walipata huduma za uchunguzi wa afya bila malipo, zikiwemo upimaji wa Kifua Kikuu (TB), UKIMWI na Homa ya Ini, pamoja na ushauri wa afya kutoka kwa wataalamu. Huduma hizo zilienda sambamba na elimu kuhusu kinga, udhibiti wa magonjwa na umuhimu wa kupima afya mapema.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Afisa wa Jamii anayehusika na masuala ya Ushirikishwaji wa Jamii, Bw. Simeon Mwanyonga, alisisitiza umuhimu wa kuwafikishia wananchi elimu sahihi kuhusu magonjwa na kuwahamasisha kupima afya zao mara kwa mara.
“Ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu magonjwa mbalimbali na umuhimu wa kupima afya zao mapema, ili kubaini hali zao na kuchukua hatua zinazostahili,” alisema Mwanyonga.
Utekelezaji wa shughuli hizo ulifanyika kwa ushirikiano kati ya Kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii, Bodi ya Ushauri ya Jamii (CAB), Mwitikio wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (MKUTA) pamoja na wataalamu wa Kifua Kikuu.
Kwa ujumla, ushiriki huo umeendelea kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika utafiti kwa kuwafikia wananchi katika mazingira yao, kuwaongezea uelewa kuhusu tafiti zinazofanyika na umuhimu wa ushiriki wao. Kupitia majukwaa kama Nanenane, utafiti unasogezwa karibu zaidi na jamii, huku wananchi wakipata fursa ya kuelewa na kushiriki katika tafiti zinazolenga kujibu changamoto za afya nchini.
Ushiriki huo ulienda sambamba na kaulimbiu ya Nanenane 2026 isemayo, “Tambua Soko, Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050,” ambapo maadhimisho ya kitaifa yalifanyika jijini Dodoma.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

Dira 2050