Tafiti za ndani ya nchi zimekuwa chanzo kikuu cha ushahidi wa kisayansi unaotumika katika kufanya maamuzi ya kisera, kuboresha huduma na kuimarisha mifumo ya afya kwa ujumla. Hayo yamesemwa leo tarehe 4 Aprili na Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti NIMR Dkt. Nyanda Ntinginya, aliyekuwa akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Tasisi ya Taifa ya Utafiti wa Maginjwa ya Binadamu (NIMR) katika mdahalo wa kitaaluma uliohusisha wadau mbalimbali wa afya, kwenye maadhimisho ya Wiki ya Afya. Maadhimisho hayo yanafanyika katika viwanja vya JKCC- Dodoma kuanzia tarehe 3 hadi 8 Aprili 2025,
Dkt. Nyanda amesisitiza nafasi muhimu ya tafiti za kisayansi katika kuboresha huduma za afya nchini Tanzania.“Kujikita katika mbinu za kitafiti kumeleta maendeleo makubwa katika kufikia malengo ya mfumo wa afya – kuanzia kwenye utoaji wa huduma, utawala bora, hadi ushirikishwaji wa wadau katika kuongeza usawa wa huduma za afya nchini Tanzania, NIMR inaendelea kuimarisha tafiti zinazotokana na mahitaji halisi ya wananchi ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika kufikia huduma bora za afya,” amesema Dkt. Nyanda.
Aidha Dkt. Nyanda amebainisha kuwa mafanikio ya kisera yanayotokana na tafiti za ndani ni pamoja na kuboreshwa kwa uwezo wa watumishi wa afya, mifumo ya usimamizi na taarifa, upatikanaji wa dawa, pamoja na mikakati ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
Mbali na kushiriki mdahalo huo wa kitaaluma, NIMR pia inashiriki kwenye maonesho yaliyoandaliwa na Wizara, bandani tuna bidhaa mbalimbali za tiba asili zinazozalishwa na kituo cha Mabibo, tunatoa elimu kuhusu mchakato wa kupata vibali vya utafiti wa afya, na kuonesha kwa vitendo namna tafiti za wadudu waenezao magonjwa kama mbu zinavyofanyika.
Ushiriki wa NIMR katika maadhimisho ya Wiki ya Afya ni sehemu ya juhudi za Taasisi katika kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la “Afya Kwa Wote”, kwa kutumia tafiti za kisayansi kama nyenzo muhimu.