Skip to content
Coat of arms of Tanzania

National Institute for Medical Research (NIMR)

Advancing Health Research, Enhancing Life

NIMR

Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) limewataka watafiti kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika vituo vya Taasisi kuongeza machapisho na ubunifu wa utafiti, ili kuzalisha ushahidi unaochangia kuboresha afya ya Watanzania na sera za afya.
Wito huo umetolewa tarehe 1 Septemba 2026, wakati Baraza lilipotembelea vituo vya NIMR Mabibo na Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujionea kwa vitendo shughuli na utendaji wa vituo hivyo, kutathmini matumizi ya miundombinu na vifaa vya utafiti, pamoja na kusikiliza maoni na changamoto za watumishi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Prof. Muhammad Bakari Kambi, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Baraza, Prof. James Mdoe, alisema NIMR ina rasilimali watu wenye uwezo na miundombinu ya utafiti inayotoa fursa kwa watafiti kuongeza uzalishaji wa maarifa na machapisho, huku akiwasisitiza kutumia fursa hizo kuongeza mchango wa NIMR kitaifa na kimataifa.
Prof. Kambi pia alisisitiza umuhimu wa kuongeza ubunifu katika tafiti na uzalishaji wa bidhaa za tiba asili, sambamba na kuimarisha masoko ya bidhaa hizo ili kuongeza matumizi na kuchangia mapato ya Taasisi. Aidha, aliwataka watumishi kutunza na kutumia kwa ufanisi uwekezaji wa Serikali katika miundombinu na vifaa vya utafiti, ikiwemo maabara na kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za tiba asili chenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.4.
Katika ziara hiyo, Baraza lilitembelea maeneo mbalimbali ya vituo hivyo na kuona shughuli za utafiti, miundombinu na vifaa vinavyotumika katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi. Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa ni maabara za kituo cha NIMR Mabibo, shughuli za utafiti wa Kifua Kikuu na UKIMWI katika katika kituo cha NIMR Muhimbili, maabara ya Kifua Kikuu iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili inayosimamiwa na NIMR kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) pamoja na Wizara ya Afya, na Maabara ya Vinasaba vya Malaria iliyopo katika Ofisi ndogo za NIMR Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, alisema NIMR Mabibo ina maabara tatu zenye mashine zaidi ya 80 zinazotumika katika tafiti na ufuatiliaji wa ubora wa dawa za tiba asili. Alisema kituo hicho pia kina mitambo takribani 15 ya uzalishaji wa dawa, ambapo mitambo tisa tayari inafanya kazi na sita ikiwa katika hatua za usimikaji.
Prof. Aboud alisema NIMR Mabibo imegundua bidhaa sita za tiba asili ambazo zipo katika hatua za awali, huku utafiti na majaribio yakiendelea. Kwa upande wa NIMR Muhimbili, alisema kituo hicho kimeendelea kutoa mchango katika kuboresha sera na miongozo mbalimbali ya afya nchini na kimataifa, ikiwemo katika maeneo ya VVU, Kifua Kikuu na magonjwa yanayohusiana nayo.
Aliongeza kuwa NIMR Muhimbili inaendelea kuongeza machapisho kupitia ushirikiano na hospitali mbalimbali, matumizi ya kanzidata za tafiti za afya na tafiti za kimfumo zinazolenga kuunganisha ushahidi kutoka tafiti mbalimbali.
Baraza pia lilipata fursa ya kukutana na watumishi wa vituo hivyo na kusikiliza maoni yao kuhusu utendaji wa kazi, changamoto wanazokabiliana nazo na maeneo yanayohitaji maboresho. Prof. Kambi aliwahakikishia watumishi kuwa changamoto zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi, huku akiwapongeza kwa kazi wanayoifanya na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya vituo hivyo.
Ziara hiyo iliwezesha Baraza kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu shughuli, mafanikio, fursa na changamoto za vituo hivyo, pamoja na kutathmini maeneo yanayohitaji msukumo zaidi katika kuimarisha utendaji wa NIMR.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

Dira 2050