NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) leo tarehe 12 Mei, 2025 imefanya kikao chake cha 16 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi katika ukumbi wa CEEMI, ofisi ndogo za taasisi zilizopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, amewataka wafanyakazi kuwajibika ipasavyo kwa kuzingatia bajeti na mpango kazi wa Taasisi, maadili ya kazi, kutunza mali za umma na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima yanayoongeza gharama za uendeshaji.

Prof. Aboud amewakumbusha wajumbe kuwa Baraza ni jukwaa muhimu linalowezesha mashirikiano kati ya menejimenti, Chama cha Wafanyakazi na Wafanyakazi wenyewe kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na utendaji wa Taasisi.

Vilevile Prof. Aboud amesema kuwa Taasisi itaendelea kuweka vipaumbele katika tafiti za magonjwa yasiyoambukiza kama Saratani na Afya ya akili, magonjwa ya kuambukiza ikiwemo ya milipuko, Usugu wa vimelea dhidi ya dawa, Tiba Asili na Tiba Mbadala na matumizi ya matokeo ya tafiti hizo katika kuboresha sera, kufanya maamuzi kwa kutumia ushahidi wa kisayansi na hatimaye kuboresha huduma kwa wananchi. Hali kadhalika, Taasisi itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato toka vyanzo vyake vya ndani na matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi na tija katika Taasisi na kuendelea kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali. Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuupa kipaumbele utafiti wa kisayansi.

Naye katibu wa Chama cha Wafanyakazi RAAWU Bwa. Joseph Sayo Mwita   akizungumza katika kikao hicho amewataka wafanyakazi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi ili kutimiza malengo ya Taasisi.

Aidha, kikao hicho kilijadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 yaliyotayarishwa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa sita wa taasisi na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025.

Kikao hicho pia kimefanya uchaguzi wa Katibu na Naibu Katibu wa Baraza, Uchaguzi wa Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Baraza Kuu la Wafanyakazi sambamba na kuhuishwa kwa Mkataba Mpya wa Baraza kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2028.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe kutoka vituo vinane vya utafiti vya NIMR nchini, pamoja na wawakilishi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi na chama cha wafanyakazi wa RAAWU Kanda ya Mashariki.