Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Copenhagen, imezindua utekelezaji wa utafiti wa miaka mitano unaolenga kuimarisha utambuzi na usimamizi wa matatizo ya afya ya akili kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), kupitia teknolojia ya kidijitali.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa CEEMI ofisi ndogo za NIMR jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza, Afya ya Akili na Majeraha kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Omary Ubuguyu ambaye alikua Mgeni Rasmi akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno F. Sunguya, amesema matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kubaini mahitaji ya wagonjwa kwa wakati na kuboresha huduma kwa watoto na makundi yenye uhitaji maalumu, wakiwemo watu wanaoishi na VVU.
Aidha Dkt. Ubuguyu amesema mpango huo ukifanikiwa utawanufaisha Watanzania wengi zaidi kwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuanzia Dar es Salaam na Mwanza na baadaye kupanuliwa katika mikoa mingine nchini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Dkt. Neema Mlole ameeleza kuwa mafunzo kupitia mfumo wa kidijitali yanaweza kusaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa afya ya akili hasa katika ngazi ya msingi na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Prof. Said Aboud amesema utafiti huo unatarajiwa kutoa ushahidi utakaosaidia kuunganisha huduma za afya ya akili na huduma za kawaida za VVU, hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma jumuishi zinazozingatia mahitaji ya wagonjwa.
Mkutano huo wa siku moja umewakutanisha watafiti kutoka NIMR, Chuo Kikuu cha Copenhagen na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi (CUHAS), pamoja na wadau wengine muhimu ambapo wamejadili mbinu za utekelezaji wa utafiti, kubadilishana uzoefu na kutoa maoni yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wake.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.









