Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) limewataka watumishi wa Kituo cha NIMR Mwanza kuendelea kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto za afya nchini, sambamba na kuhakikisha matokeo chanya ya tafiti hizo yanaleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Prof. James Mdoe, wakati wa ziara ya Baraza hilo katika Kituo cha NIMR Mwanza, ambapo amewataka watumishi kutekeleza Mpango Mkakati wa NIMR unaokwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Prof. Mdoe amesema ni muhimu kuongeza tafiti zinazohusu matumizi ya Akili Unde (AI) katika kuboresha utoaji wa huduma za afya na kutoa ushahidi wa kisayansi utakaosaidia watunga sera na wafanya maamuzi kubaini namna teknolojia hiyo inavyoweza kutumika katika mazingira ya Tanzania.
Aidha, amewahimiza watumishi kutumia utaalamu wao kutoa huduma za ushauri elekezi (consultancy services), akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza maarifa, kipato cha watumishi na taasisi, pamoja na kuchangia maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, amesema kituo hicho kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha miundombinu ya utafiti, maabara za kisasa na uwezo wa rasilimali watu.
Ameeleza kuwa tafiti za kituo zimechangia kuboresha tiba na kinga ya magonjwa mbalimbali yakiwemo malaria, VVU/UKIMWI, saratani ya shingo ya kizazi, kifua kikuu, kichocho na minyoo ya tumbo.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2025/2026, kituo kilitekeleza miradi 33 ya utafiti, kikachapisha zaidi ya machapisho 50 ya kisayansi na kuandaa vijarida sera viwili (2)
Katika ziara hiyo, wajumbe wa Baraza walitembelea Maabara na kitengo cha Mbu (Insectary), Kituo cha Afya kinachomilikiwa na NIMR pamoja na eneo la taasisi, ili kujionea hali halisi ya miundombinu na shughuli zinazotekelezwa.
Ziara hiyo imelenga kujionea shughuli za utafiti na huduma zinazofanywa na Kituo cha NIMR Mwanza, kubaini changamoto zinazowakabili watumishi na kutafuta namna ya kuzitatua ili kuwezesha kituo kutekeleza majukumu yake na kufikia malengo yaliyowekwa.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.








