Skip to content
Coat of arms of Tanzania

National Institute for Medical Research (NIMR)

Advancing Health Research, Enhancing Life

NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imewataka watumishi wapya kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, uwajibikaji, nidhamu na ubora wa kazi ili kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu na kufikiwa kwa malengo ya Taasisi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali ya utumishi wa umma kwa watumishi wapya, yanayofanyika kuanzia tarehe 19–21 Oktoba 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said S. Aboud, amewataka watumishi hao kuhakikisha kuwa majukumu yao ya kila siku yanaendana na Mpango Mkakati wa Taasisi, akisisitiza kuwa shughuli zote, zikiwemo tafiti, huduma za maabara na kazi za kiutawala, zinapaswa kuchangia katika kufikiwa kwa malengo ya kimkakati ya NIMR.
Prof. Aboud amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na ubora, akieleza kuwa mafanikio ya kisayansi na kitaasisi yanahitaji kujituma, nidhamu, uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa kila jukumu.
Aidha, amewataka watumishi hao kuepuka vitendo vinavyoweza kudhoofisha tija na kuathiri taswira ya Taasisi, ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya muda wa kazi, matumizi ya vilevi mahali pa kazi na kushiriki katika shughuli binafsi kama kamari na ubashiri wa michezo wakati wa saa za kazi.
Kwa upande wake, Fute Martin, mwezeshaji kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amewasisitiza watumishi hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. Pia ameeleza umuhimu wa kuelewa haki na wajibu wao pamoja na kuzingatia maadili, weledi na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.
Naye Anicet Michael Swai, mwezeshaji kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), amewahimiza watumishi wapya kusajiliwa na kujiunga na Mfuko huo ili kujiwekea msingi imara wa maisha yao ya baadaye. Katika mafunzo hayo, amewapatia elimu kuhusu uanachama, aina za mafao yanayotolewa na Mfuko pamoja na faida za kuwa mwanachama wa hifadhi ya jamii katika kujihakikishia ustawi wa kifedha wakati wa utumishi na baada ya kustaafu.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanalenga kuwajengea watumishi wapya uelewa kuhusu mfumo wa utumishi wa umma, maadili ya kazi, taratibu za kiutawala, haki na wajibu wao pamoja na mwelekeo wa kimkakati wa NIMR, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya utumishi bora wa umma.
Jumla ya watumishi wapya 43 kutoka kada mbalimbali, zikiwemo za watafiti, watunza kumbukumbu, madereva, maafisa rasilimali watu, wataalamu wa maabara na wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), wanashiriki mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dodoma.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.

Dira 2050