NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa kushiriki Mkutano wa 13 wa Kitaaluma wa Chama cha Makatibu Muhtasi na Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA), uliofanyika katika Ukumbi wa Ngurdoto, mkoani Arusha, kuanzia tarehe 18 hadi 23 Mei, 2026.
Mkutano huo uliwakutanisha makatibu muhtasi na waandishi waendesha ofisi kutoka taasisi mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili mabadiliko ya kiteknolojia, maendeleo ya kitaaluma pamoja na kuimarisha maadili, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi.
Katika mkutano huo, NIMR iliwakilishwa na makatibu muhtasi wanane kutoka Makao Makuu na katika vituo vyake nchini ambao ni Rukia Mbwana (Makao Makuu Dodoma), Dalin Chimbonaga (Mabibo), Charity Msangi (Tanga), Sikuzani Masaka (Tabora), Jacquline Mtambi (Makao Makuu Dodoma), Asia Mwanaupanga (Mbeya), Tabitha Temhanga (Dodoma) na Laika Tibishubwamu (Mwanza).
Ushiriki wa watumishi hao unaakisi dhamira ya dhati ya ya taasisi katika kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuongeza tija, weledi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Mgeni rasmi kwenye mkutano huo alikuwa Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye alisisitiza umuhimu wa ubunifu, uwajibikaji, uadilifu na ufanisi kama msingi wa maendeleo endelevu katika maeneo ya kazi.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni: “Ubunifu, Uwajibikaji, Uadilifu na Ufanisi ni Mojawapo ya Misingi Imara ya Maendeleo Endelevu Kwenye Utendaji Kazi.”
Kupitia ushiriki huo, watumishi wa NIMR wanapata fursa ya kujifunza mbinu mpya za utendaji kazi, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma pamoja na kujengewa uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia katika mazingira ya kisasa ya kazi.
Ushiriki wa NIMR katika mkutano huo unaendelea kudhihirisha maono ya taasisi ya kuimarisha utendaji kazi kwa kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu, weledi na utoaji wa huduma bora kwa jamii.

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.