NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa vitendo kwa kutoa huduma za afya bure kwa wananchi katika vituo mbalimbali nchini, hatua iliyowezesha wengi kutambua hali zao za kiafya na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa.
Maadhimisho ya kitaifa ya Mei Mosi mwaka 2026 yamefanyika mkoani Njombe yakiongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sanjari na maadhimisho hayo, vituo vya NIMR nchini vilishiriki kwa kutekeleza shughuli za kijamii, hususan utoaji wa huduma za afya bure kwa wananchi.
Huduma zilizotolewa ni pamoja na vipimo vya malaria kwa kutumia mRDT, sukari kwenye damu, shinikizo la damu, pamoja na vipimo vya uzito na urefu. Wananchi pia walipatiwa elimu ya afya kuhusu magonjwa mbalimbali, hasa malaria, ili kuwajengea uwezo wa kujikinga na kutambua dalili mapema.
Katika vituo mbalimbali ikiwemo Tanga, Amani, Mwanza na Mbeya, wananchi walijitokeza kwa wingi kupatiwa huduma hizo. Katika viwanja vya Mkwakwani mkoani Tanga, baadhi ya wananchi walieleza kufurahishwa na huduma hizo, wakisema zimewasaidia kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua mapema.
“Huduma hizi zimetusaidia sana. Wengi wetu hatupati nafasi ya kupima afya mara kwa mara, lakini leo tumepata fursa ya kujua hali zetu,” alisema mmoja wa wananchi aliyepata huduma hizo.
Sanjari na utoaji wa huduma, watafiti kutoka vituo vya NIMR walitoa elimu na kuonesha shughuli mbalimbali za utafiti zinazotekelezwa na taasisi hiyo, ikiwemo tafiti kuhusu mbu na ugonjwa wa malaria. Lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mchango wa tafiti katika kuboresha afya na kudhibiti magonjwa.
Aidha, wafanyakazi hodari wa NIMR kwa mwaka 2026 walitambuliwa katika maadhimisho ya kitaifa kwa kupatiwa vyeti na zawadi, ikiwa ni kuthamini mchango wao katika maendeleo ya taasisi na sekta ya afya nchini.
Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: “Kazi Zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu Katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.