Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) leo tarehe 21 Aprili 2026, imefanya Mkutano wa 17 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kujadili na kupitisha Mpango Mkakati wa Taasisi wa miaka mitano (2026–2031) pamoja na Mpango na Maoteo ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Mpango Mkakati huo na bajeti hiyo vimeandaliwa kwa kuzingatia Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti, Mpango Mkakati wa NIMR, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2025–2030, pamoja na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Wizara ya Fedha, Sera za Kisekta na maelekezo ya Wizara ya Afya.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi ya taasisi ili kila mfanyakazi anapotekeleza majukumu yake afahamu kwa uwazi matarajio ya Mpango Mkakati. Aidha, inalenga kuhakikisha wafanyakazi wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na utekelezaji wa malengo ya taasisi.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, amesema Baraza hilo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wafanyakazi na Menejimenti katika kujadili na kutoa ushauri kuhusu usimamizi wa kazi, rasilimali watu na mazingira bora ya kazi.
Prof. Aboud amesema NIMR inaendelea na juhudi mbalimbali za kuongeza mapato ya taasisi ikiwemo mpango wa kuanzisha Kampuni Tanzu (Spin Off Company) itakayorahisisha mashirikiano na wadau na kuongeza mapato kwa taasisi na Serikali, kujenga jengo la ofisi Dodoma, kuboresha miundombinu ya kufanyia kazi, kutenga fedha za kufanya tafiti kwa ajili ya watafiti wachanga (Early Career Research Scientists) na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Aidha, amesema kupitia Kituo cha Mabibo, NIMR inaendelea kuzalisha dawa za tiba asili sambamba na kuendesha tafiti mbalimbali za kisayansi zinazolenga kuboresha afya za wananchi.
Akitaja baadhi ya mafanikio ambayo Taasisi imeipata katika mwaka mmoja uliopita, Prof Aboud alisema Taasisi imeendelea kufanya tafiti ambazo zimetoa matokeo chanya katika kuboresha sera na huduma, kukarabati miundombinu ya vituo vyake, kununua vitendea kazi kwa ajili ya watumishi, kusimika mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi na tija, kuhamishia Makao Makuu ya Taasisi Dodoma, kuwapatia ofisi kituo cha NIMR Muhimbili badala ya kuendelea kupanga ili kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi, kuzalisha dawa za tiba asili na kuchangia katika huduma jumuishi zinazotolewa katika Hospitali za Rufaa za Mkoa 14 na kuboresha maslahi ya wafanyakazi kupitia motisha. Katika hotuba yake, Prof. Aboud pia amewakumbusha wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kutumia muda wa kazi ipasavyo na kutunza rasilimali za taasisi ili kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu.
Mkutano Mkuu wa 17 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi umewakutanisha wajumbe kutoka vituo vyote vya NIMR pamoja na Makao Makuu, kwa lengo la kujadili kwa kina masuala mbalimbali yatakayosaidia kuimarisha utendaji wa taasisi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Ushauri, Habari na Utafiti (RAAWU) akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa RAAWU Taifa, Bw. Simon Mbai pamoja na Katibu wa RAAWU Kanda ya Kati, Bi. Staile Kiko.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Ut elit tellus, luctus nec ullamcorper mattis, pulvinar dapibus leo.





