NIMR

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Bw. Aretas Lyimo ameipongeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kuunga mkono mapambano dhidi ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa kufanya tafiti zenye tija – kuibua kifua kikuu kwa waraibu wa dawa za kulevya.
Kamishna Lyimo ametoa pongezi hizo leo katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya Duniani alipotembelea banda la NIMR katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma ambapo ametoa cheti cha ushiriki kama mshirika muhimu katika kuunga mkono juhudi za kitaifa na kimataifa za kutokomeza janga la dawa za kulevya kupitia tafiti zenye tija.
Katika maadhimisho hayo, NIMR imetoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kuhusu tafiti za afya na kuonesha shughuli zinazotekelezwa katika vituo vyake mbalimbali vya utafiti nchini.
Aidha Mtafiti Mwandamizi Dkt. Lilian Tina Minja, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NIMR amesema katika utafiti walioufanya wamebaini changamoto za uibuaji wa kifua kikuu katika ngazi ya jamii kwa kupitia makundi rika ikiwa ni pamoja na uhamaji wa mara kwa mara wa waraibu wa dawa za kulevya, unyanyapaa na kujihusisha kwa waraibu wa dawa za kulevya na tabia hatarishi zinazochangia kuongeza maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Kassim aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo maadhimisho hayo yalibebwa na Kauli mbiu inayosema “Wekeza kwenye Kinga na Tiba Dhidi ya Dawa za Kulevya”.