Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud, amewapongeza watumishi wa NIMR kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uwajibikaji na uadilifu. Vilevile, ameipongeza timu ya maandalizi ya NIMR kwa kufanikisha maonesho yenye mafanikio makubwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025.
Prof. Aboud ametoa pongezi hizo leo tarehe 22 Juni 2025, alipotembelea banda la NIMR katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma ambako maadhimisho hayo yanaendelea kufanyika.
“Watumishi wenzangu, tuendelee kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya Serikali. Tuuishi uadilifu kwa vitendo” amesema Prof. Aboud.
Banda la NIMR limeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo elimu kuhusu tafiti za afya na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za tiba asili zinazozalishwa na kituo cha NIMR Mabibo. Banda hilo limeendelea kuvutia watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wananchi wa kawaida, wanafunzi, watumishi wa umma na viongozi wa Serikali.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa maalumu linalowezesha taasisi za umma kuonesha huduma wanazotoa kwa wananchi pamoja na mafanikio yaliyopatikana. Pia ni fursa ya kuhamasisha uwajibikaji, weledi na utoaji wa huduma bora kwa umma.