Katika jitihada za kuboresha huduma za afya kwa wananchi, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kupitia Mradi wa utafiti wa PENPLUS, imeboresha jengo la kutolea huduma za kibingwa kwa magonjwa yasiyoambukiza katika Hospitali ya Mji Kondoa, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na kuboresha matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji wa huduma za kibingwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi jengo hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Mkurugenzi wa Taarifa na Kurekebu Tafiti ambaye pia ni Mtafiti Kiongozi wa mradi huo Dkt. Mary Mayige amesema kuwa, kupitia mradi wa PENPLUS wamekuwa wakitoa mafunzo kwa madaktari pamoja na kuwezesha Hospitali za Wilaya ili kuweza kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za ziada.
Aidha Dkt. Mayige amesema kuwa katika mradi wa PENPLUS wamechagua magonjwa ambayo yanaathiri zaidi watoto kama vile kisukari aina ya Kwanza, selimundu, pamoja na ugonjwa wa moyo unaoathiri watoto (Rheumatic Heart Disease).
“Kwa hiyo hawa watoto kwa muda mrefu wamekua wanashindwa kupata huduma hizi za kila siku katika hospital za wilaya kwa sababu huduma zao zinahitaji ubobezi kidogo, wengi walikua wanalazimika kusafiri kwenda Hospitali za Rufaa za Mkoa na za Kanda ili kuweza kupata matibabu, kulikuwa na changamoto kwa sababu ya umbali mrefu na watoto walikuwa hawawezi kwenda shule.” Ameeleza Dkt. Mayige.
Akiishukuru NIMR baada ya kukabidhiwa jengo hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitaili ya Mji Kondoa Dkt. Ramadhan Lwambangulu amesema kuwa Mradi wa PENPLUS umesaidia kukuza uelewa kwa jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza uwezo na uzoefu kwa madaktari wa hospitali, hivyo ukarabati wa jengo hilo utasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Ameongeza kuwa utoaji wa huduma hizo ni gharama kubwa sana hasa kwa mwananchi mwenye kipato cha chini hivyo ujio wa mradi wa utafiti wa PENPLUS umewasaidia wanachi kuepukana na gharama hizo ambazo ziliwafanya washindwe kupata matibabu.
“Zile huduma za kibingwa ambazo angezipata katika hospitali za rufaa za mkoa na kanda anazipata katika Hospitali ya Wilaya kutokana na uwepo wa madaktari mabingwa ambao wanakuja kwenye kliniki ya PENPLUS, tunashukuru sana kwa hilo imetusaidia kuongeza hamasa kwa jamii yetu”. Amesema Dkt. Lwambangulu.
Akizungumzia Mradi huo Mkazi wa Kondoa Mji Gema Aloyce Kilumanga ameishukuru NIMR kupitia Mradi wa PENPLUS kwa kuwaletea huduma za matibabu karibu na bila gharama yoyote kwani kabla ya ujio wa PENPLUS walilazimika kufuata huduma hizo mbali na kwa gharama wasizomudu katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na katika hospitali nyingine za Kanda na Taifa.
“Kabla ya hapa tulilazimika kupata huduma sehemu za mbali Dodoma, kutafuta dawa kwa gharama kubwa, lakini baada ya huduma hii kufika hapa tumeweza kupata huduma nzuri za vipimo na dawa na pia mwanangu alikua hawezi kucheza na wenzake, kwenda shule, alikua na homa za mara kwa mara, alikua mgonjwa wa kila siku, baada ya kupata huduma, mtoto huyu sasa hivi anaweza kusoma, kuendesha baiskeli, anacheza mpira, wingi wa damu ya umekuwa wa kawaida sio kama zamani, tunaishukuru sana NIMR” Amesema Gema Kilumanga Mkazi wa Kondoa Mji.
Naye mkadarasi aliye karabati jengo hilo Christopher Kaijage amesema jengo hilo lilikuwa katika hali isiyokuwa ya matumizi, NIMR kupitia mradi wa PENPLUS wamewezesha ukarabati kama vile miundombinu ya maji, umeme, dari, kubadili madirisha na milango, kupaka rangi, kuweka marumaru, kugawanya vyumba na kuweka samani mbalimbali na sasa wamekabidhi likiwa katika hali ya upya na tayari kwajili ya matumizi. Jukumu kubwa la
Mradi wa PENPLUS ni kuongeza ufanisi na uwezo kwa Hospitali za Wilaya kutoa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa zaidi kwa kuongeza vifaa, miundombinu, kutoa mafunzo na kuongeza madaktari wabobezi katika kutoa huduma za magonjwa yasiyoambukiza.